Dk. Shein azungumza na mabalozi wa nchi tatu IKULU Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein  amekutana na  kufanya mazungumzo na mabalozi wa nchi za Kuwait, Ethiopia na Misri.
Katika mazungumzo yalijikita zaidi katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano sambamba na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi za kujiletea maendeleo.
Mazungumzo hayo yalifanyika kwa nyakati tofauti ikulu mjini Zanzibar ambapo mabalozi hao walifika kwa ajili ya kujitambulisha kwa Dk. Shein.
Miongoni mwao ni Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Mubarak Mohammed, Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania, Yonas Yosef na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Gaber Mohamed.
Katika mazungumzo yao Mabalozi hao walipongeza mafanikio yaliofikiwa Zanzibar na kuahidi kuendelea kuyaunga mkono huku wakitumia fursa hiyo kutoa pongezi maalum kwa Dk. Shein na wananchi wa Zanzibar kwa kufanikisha sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza na Balozi wa Kuwait, Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na kuupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi  wa Kuwait kwa kuiunga mkono Zanzibar.
Alisema  Kuwait imekuwa ikitoa ushirikiano kwa Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu na kilimo huku akiwakaribisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar.
Nae, Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Mubarak Mohammed alieleza azma ya nchi yake ya kuendelea kushirikiana na Zanzibar kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo.
Dk. Shein pia, alifanya mazungumzo na  Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Yonas Yosef ambapo katika mazungumzo hayo, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein mafanikio yaliofikiwa na nchi yake kiuchumi, kisiasa na kijamii ikiwa ni pamoja na kukua kwa shirika  la ndege la ‘Ethiopia Airlines’, pamoja na kurejesha uhusiano kati ya Ethiopia na nchi jirani ya Eritrea.
Alimueleza Dk. Shein kuwa kuimarika kwa sekta ya usafiri kupitia kampauni ya ndege ya Ethiopia Airlines, kutaongeza idadi ya watalii wanaofika Zanzibar pamoja na kutoa huduma bora za usafiri kwa wananchi wa pande mbili hizo.

Comments