Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema
mzee Karume alitekeleza mambo mbali mbali, ikiwemo elimu, huduma za
afya, miundombinu ya barabara, pamoja na kuimarisha huduma za wazee kwa
kuwajengea nyumba za makaazi na wananchi kujengewa nyumba za kisasa za
maendeleo.
“Serikali imejitahidi kuhakikisha inaendeleza yale yote yaliyoasisiwa
na mzee Karume, tayari huduma nyingi za maendeleo zinatekelezwa,”
alisema.
Alisema serikali tayari imejenga mtandao wa barabara zenye urefu wa
kilomita 1261 kwa Unguja na Pemba, ikiwa ni kuyaenzi mapinduzi ya
Zanzibar.
Alisema serikali inayoongozwa na Dk. Shein, itaendelea kuwapatia
wananchi wake maendeleo bora, ikiwa ni ahadi ya chama cha ASP
ikizingatiwa barabara ya Wawi Mabaoni itaondosha tatizo la msongamano wa
gari kwenye barabara kuu ya Chake Chake-Wete.
Aidha aliwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza barabara hiyo, ili
iweze kudumu pamoja na kuacha tabia ya kuchoma matairi barabarani.
Aliishukuru kampuni ya MECCO kwa kukamilisha kwa wakati ujenzi wa barabara hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Dk. Sira Ubwa
Mwamboya, alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutaharakisha maendeleo ya
kiuchumi kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla, aliwaomba
wananchi wa Wawi kuhakikisha wanaitunza barabara hiyo pamoja na madereva
kuacha tabia ya kuendesha vyombo vyao kwa mendo wa kasi.
Katibu Mkuu wizara hiyo, Mustafa Aboud Jumbe, alisema tayari kilomita 1261 za barabara zimejengwa Zanzibar baada ya mapinduzi.
Zanzibarleo.
Comments