Waziri wa Elimu Zanzibar awataka walimu wakuu kukagua walimu wanao wasimamia.

Image may contain: 2 people, people standing and textWAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amewataka walimu wakuu wa skuli za sekondari nchini kufanya ukaguzi wa kazi za walimu wao ili kupata maendeleo bora ya elimu na ufaulu mzuri kwa wanafunzi.

Akifungua mkutano wa sita wa Jumuiya ya walimu wakuu wa skuli za sekondariZanzibar JUWASEZA katika ukumbi wa skuli ya sekondari ya Mohamed Juma Pindua Mkoani Pemba, Mhe Riziki amesema suala la ufundishaji katika skuli zote, walimu wakuu ndio viongozi na ndio wakaguzi wa kwanza, hivyo ni vyema kulizingatia kwa kina suala hilo ili kuwapatia watoto haki yao ya msingi.

Amefahamisha kuwa bila ya kufundishwa watoto ipasavyo,taifa litazalisha wataalamu wachache na wasiokuwa na uwezo, hivyo itapelekea kukosekana kwa maendeleo endelevu hapa nchini.

Akizungumzia kuhusiana na kanuni na muongozo wa kazi Mhe Riziki amesema Wizara inatambua kuwa kila Skuli inayo muongozo na kanuni zao lakini kuna baadhi ya skuli hawaifuati ipasavyo na kupelekea shughuli za utendaji wa kazi za skuli hizo kuharibika.

Hivyo Mhe Riziki amewataka walimu wakuu wote kuhakikisha miongozo hiyo inafuatwa ipasavyo ili kila mtu afahamu wajibu wake kwa lengo la kuleta ufanisi wa kazi zao za kila siku.

Kuhusu suala la ruzuku Mhe Riziki amesema Wizara inafahamu lengo la kupatiwa ruzuku, hivyo amewataka JUWASEZA kuhakikisha kuwa ruzuku wanazoapatiwa zinatumika kwa mujibu wa mpango kazi na si kuitumia kinyume na utaratibu, ambapo amesema sheria Kali zitachukuliwa kwa yeyote atakaebainika kwenda kinyume na malengo ya ruzuku hizo.

Aidha Mhe Riziki amesema kuhusu suala uvujishaji wa mitihani amewataka walimu wakuu kuzungumza na walimu wao kutojishirikisha na masuala hayo kwani ni kukosa uzalendo wa nchi yao.

Wakisoma risala yao Naibu Katibu wa Jumuiya ya walimu wakuu wa skuli za sekondari kanda ya Unguja Bi Khadija Said Kassim amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata ikiwemo kuendesha mafunzo ya masomo ya sayansi kwa walimu sekondari, lakini bado wana matatizo mbalimbali ikiwemo upungufu wa viwanja vya michezo katika skuli.

Mkutano wa sita wa Jumuiya ya walimu wakuu wa JUWASEZA umefanyika ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni " usimamizi bora wa ruzuku kwa walimu wakuu ndio chachu ya maendeleo ya elimu Zanzibar.Image may contain: 9 people, crowd
 Image may contain: 5 people

Comments