Waasi wa zamani wa FDLR waunganishwa na familia zao nchini Rwanda.

Waasi wa zamani wa FDLR waunganishwa na familia zao nchini Rwanda Waasi wa zamani wa harakati ya FDLR wamesafrishwa hadi nchini Rwanda wakiwa na familia zao zinazowategemea wakitokea katika misitu inayopatikana katika mikoa ya Equateur, Kanyabayonga, Walungu na Kisangani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo wengi kati yao waliishi huko tangu mwaka 1994. 

Kamisheni inayohusika na kuwakusanya waasi hao imesema kuwa waasi hao waliorejea nyumbani wote wamekusanywa katika kituo cha Mutobo ambapo watapatiwa mafunzo ya kiraia kabla ya kuunganishwa na jamii zao za asili.

Baadhi ya wanamgambo hao wa zamani waliozungumza na gazeti la Teh New Times la nchini Rwanda wamesema kwamba, walikuwa wanahofia usalama wao nchini Rwanda kwa sababu walipatiwa taarifa za uongo na makamanda wao na watu wengine ambao wamekuwa na maslahi na kunufaika na kuendelea kuwepo kwa kundi hilo la waasi.

Itakumbukwa kuwa kwa miaka kadhaa sasa Rwanda imekuwa ikiendesha zoezi la kuwaunganisha na familia zao waasi hao na hadi hivi sasa imeshawaunganisha na familia hizo zaidi ya waasi wa zamani elfu kumi huku kila muasi akipatiwa mtaji wa kuanzia maisha wa faranga za Rwanda elfu sitini sambamba na kupatiwa mafunzo ya ujuzi wa maisha kwa ajili ya kuanza maisha mapya uraia.
parstoday.

Comments