Mfumko wa bei waongezeka.

MFUMKO wa bei wa mwaka ulioishia ulioishia Novemba 2018, umeongezeka hadi asilimia 4.4 ikilinganishwa na asilimia 3.7 iliyorikodiwa mwaka ulioishia Oktoba 2018.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Khamis Abdul-rahman Msham, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana.

Alisema, kiwango cha mfumko wa bei cha vyakula na vinywaji visivyo na vilevi kiliongezeka hadi asilimia 3.4 mnamo Novemba 2018 kutoka asilimia 2.6 mwezi Oktoba 2018.

Aidha, alisema, faharisi za bei ziliongezeka hadi 108.0 mnamo Novemba 2018 ikilinganishwa na 103.4 zilizoripotiwa Novemba 2017.

Alisema, kiwango cha mfumko wa bei wa mwaka kwa vyakula kiliongezeka hadi asilimia 3.5 kwa mwaka ulioishia Novemba 2018, ikilinganishwa na asilimia 2.7 kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2018.

Mkuu huyo, alisema, faharisi za bei za vyakula ziliongezeka hadi 105.0 mnamo Novemba 2018 ikilinganishwa na 101.5 iliyoripotiwa Novemba 2017.

Vilevile kiwango cha mfumko wa bei wa mwaka kwa bidhaa zisikuwa za vyakula kiliongezeka kwa asilimia 5.2 mwezi Novemba 2018 ikilinganishwa na asilimia 4.5 mwezi Oktoba 2018, huku faharisi za bei zikiongezeka hadi 110.3 mwezi huo wa Novemba, ikilinganishwa na 104.9 kwa mwezi Novemba 2017.

Bidhaa zilizochangia kuongezeka kwa mfumko wa mwaka zilikuwa ni mchele wa mapembe (21.4%), samaki (2.5%), saruji (2.9%), mafuta ya taa (21.2%), petrol (13.5%) na diseli (9.1%).

Kwa upande wa mfumko wa mwezi Novemba 2018, kiwango kilipungua kwa asilimia 0.3 asilimia ikilinganishwa na asilimia 0.4 mwezi Oktoba 2018.

Pia mfumko kwa bei wa mwezi kwa vyakula na bidhaa zisizo na vilevi mwezi ulioishia Novemba 2018, ulipungua wa asilimia hasi 1.5 ikilinganishwa na asilimia 0.9 kwa mwezi Oktoba 2018.

Alisema, kushuka kwa kasi ya mfumko wa mwezi kulichangiwa na bidhaa kama vile mchele wa Mbeya (2.4%), Sembe (5.5%), samaki (5.8%), ndizi za mkono mmoja (10.3%) na sukari (0.2%).

Mkuu wa Takwimu za Kiuchumi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu, Abdulrauf Ramadhan Abeid, alisema, kwa ujumla katika nchi tatu za Afrika Mashariki mfumko bado unaendelea kubakia chini ya tarakimu moja na hivyo kwenda vizuri kiuchumi.

Alisema, mfumko wa bei wa Kenya ulifikia alimia 5.58 mwezi Novemba kutoka 5.53 mwezi Oktoba wakati Uganda upo asilimia 3.0.

Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Uchumiya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Suleiman Simai Msaraka, alisema, kiuchumi bado kasi ya mfumko inaendelea vizuri na haijaathiri kimaisha, ikizingatiwa bidhaa zilizoongezeka bei zinatoka nje na nchi kutokuwa na uwezo wa kuzuia bei kulinganisha na soko la kimataifa.

Zanzibarleo.

Comments