MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa usafi wa mazingiara Disemba 31, 2018 ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 55 ya mapinduzi ya Zanzibar.
Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya mjini, Said Juma Ahmada, alieleza hayo wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Malindi.
Alisema baraza hilo litatoa vifaa vyote vinavyohitajika katika usafi wa mazingira, hivyo aliwaomba wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kuunga mkono kampeni hiyo.
Katika hatua nyengine, aliwaomba wakaazi wa nyumba za maendeleo Michenzani, Kilimani na Kikwajuni pia kushiriki katika zoezi hilo ili kuweka mazingira yao katika hali ya usafi.
Alisema pamoja na juhudi zinazochukuliwa na baraza hilo za kuimarisha usafi, maeneo hayo bado hayaridhishi kutokana na baadhi ya wakaazi kutoona umuhimu wa usafi.
Alisema kama wananchi watajenga utamaduni wa kutunza na kuweka mazingira safi, inaweza kusaidia kupunguza maradhi ya kuambukiza.
“Usafi ni tabia njema inayomstahiki kila mtu na sio suala la baraza la manispaa pekee, hivyo tujitokezeni kwa wingi kuunga mkono kampeni hii,”alisema.
Zanzibarleo.
Comments