Z’bar, Morocco kuimarisha ushirikiano.

MOROCCO imeshauri kuwepo utamaduni wa kutembeleana kati ya watendaji wa mahakama za nchi hiyo na Zanzibar.

Waziri wa Sheria wa Morocco, Mohammed Auajjar, alisema hatua hiyo itawezesha watendaji wa mahakama hizo kujifunza baina yao na kubadilishana uzoefu juu ya namna bora ya utekelezaji wa majukumu yao.

Alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman.

Mawaziri hao wako nchini India kuhudhuria mkutano wa majaji wakuu wa dunia ulioanza Novemba 16, katika jimbo la Utter Pradesh.

Katika mazungumzo yao, walitambua urafiki na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Morocco, ambapo wote walikubaliana haja ya kuuimarisha zaidi kwa maslahi ya nchi zao.

Kwa upande wake, Waziri Haroun alimueleza Waziri Auajjar, kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ipo tayari kwa ushirikiano huo akisema utaongeza ujuzi na maarifa kwa watendaji wa mahakama za pande zote mbili.

Viongozi hao kwa pamoja, walisema ni vyema utaratibu huo uanzie katika mahkama ya kadhi hasa ikizingatiwa kuwa Morocco kwa sasa inatumia kiarabu kama lugha ya mahakama.

Hata hivyo, Waziri Auajjar alisema Morocco iko katika maandalizi ya kuanzisha mafunzo ya muda mfupi kwa ajili ya watendaji wa mahakama yatakayotolewa kwa lugha ya kiingereza.

Aliiomba Zanzibar pia itumie fursa hiyo kupeleka watendaji wa mahakama zake nchini Morocco kwa ajili ya kunufaika na mafunzo hayo.

Waziri Haroun alitumia fursa hiyo kuialika mahakama ya Morocco kufanya ziara Zanzibar ili kujifunza mfumo wa mahakama ikiwemo ya mahakama ya kadhi ambayo husimamia mambo yote yanazohusu mambo ya kiislamu.

Katika hatua nyengine, Waziri Auajjar alisema nchi yake imeanzisha mkutano wa kimataifa wa majaji ambao mwaka huu ulifanyika Aprili na kuwakutanisha watendaji wa mahkama na wengine kutoka taasisi za sheria kwenye nchi mbalimbali.

Alimkaribisha Haroun na ujumbe wake kuhudhuria katika mkutano kama huo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2019.

Alisema mkutano huo uitwao ‘Marrakesh International Justice Conference, unalenga kujadili na kutoa maazimio mbalimbali ya msingi katika uimarishaji utawala wa sheria na utawala bora.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini India, Baraka Luvanda, Naibu Katibu Mkuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utawala Bora, George Kazi na Mrajisi wa mahakama kuu Zanzibar, Mohamed Ali Mohammed.

Kwa upande wake, Waziri Auajjar aliambatana na Balozi wa Morocco nchini India, Mohamed Malik, Rais wa mahakama ya juu Morocco, Wakidi Abdulazizi, pamoja na watendaji wengine wa mahakama na serikali.

Zanzibarleo.

Comments