WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Wizara zinazohusika na masuala ya
viwanda, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa
pamoja na sekta binafsi watambue na waondoe vikwazo na urasimu dhidi ya
ujenzi na ustawi wa viwanda nchini.
Pia,
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage ampelekee taarifa ya hatua iliyofikiwa juu ya kampuni ya
Budget Motors walioomba kibali cha kutengeneza na kuunganisha bodi za
mabasi tangu mwaka jana na hawajajibiwa.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Novemba 3, 2018) wakati akifunga
wiki ya maonesho ya viwanda yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba
katika kata ya Picha ya Ndege, Kibaha mkoani Pwani. Amesena uwepo wa
viwanda nchini unatoa ajira nyingi.
“Serikali
ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeamua
kujenga uchumi wa viwanda utakaokuwa mhimili mkuu wa maendeleo ya Taifa
na wananchi, hivyo itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha ajenda
ya ujenzi wa viwanda inafanikiwa.”
Amesema
katika kupunguza vikwazo na kuboresha sera nchini, Rais Dkt. Magufuli
ameweka msukumo wa kutosha ili kurahisisha na kuondoa ukiritimba kwenye
shughuli zote za kibiashara, lakini pia katika kuboresha sera za Taifa
za kodi ili kulinda viwanda vya ndani
Waziri
Mkuu amesema umuhimu wa viwanda umetokana na Ilani ya uchaguzi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 ambayo inaielekeza Serikali
kuweka nguvu katika ujenzi wa viwanda ili kufikia malengo ya Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
Amesema
kwa msingi huo, Rais Dkt. Magufuli alitoa msukumo wa sekta binafsi
nchini kuanzisha viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini
kutokana na mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili, vikiwemo
viwanda vya nguo, sabuni, korosho na matunda.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa uwepo wa viwanda nchini utasaidia kuongeza wigo wa
mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali. “Huu ndio mwelekeo
wa Serikali ya awamu ya tano unaolenga kuifikisha nchi kwenye uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.”
Kuhusu
suala la kampuni ya Budget Motors, Wiziri Mkuu amesema ifikapo Ijimaa
(Novemba 9, 2018) Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji awasilishe
taarifa kuhusu suala hilo la kibali. “Huu ni urasimu, ni bora apewe
atengeneze na akikosea arekebishwe.”
Kampuni
ya Budget Motors inadai kuwa iliomba kibali cha kuwa na uthibitisho wa
kutengeneza na kuunganisha bodi za mabasi kutoka Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), kwa takribani mwaka mmoja bila ya kujibiwa. Walitoa
malalamiko hayo kwa Waziri Mkuu alipotembelea banda lao.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa rai kwa taasisi zenye miradi
mbalimbali nchini pamoja na wananchi kuthamini na kuzitumia bidhaa
zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini zikiwemo na za viwanda vya
mkoa wa Pwani kwani zina viwango vya ubora.
“Wakati
natembelea mabanda kwenye maonesho haya nimeshuhudia bidhaa nyingi
nzuri na zenye ubora. Nimeona wazalishaji wa saruji, mabati, nondo,
marumaru, mabomba ya plastiki, chuma, zana za kilimo, vyakula, vinywaji
na vifungashio.”
Waziri
Mkuu amesema kupitia maonesho hayo ya viwanda vilivyopo katika mkoa wa
Pwani vimeudhihirishia umma kuwa vina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa
zilizo bora na hata kuzidi zile zinazoingizwa kutoka nje, amewahamasisha
wananchi kutumia bidhaa za ndani.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo
ameiagiza mikoa yote nchini kuhakikisha inatumia bidhaa zinatengenezwa
na viwanda vya ndani katika miradi mbalimbali ya ujenzi wanayoitekeleza
kama ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya.
Amesema
Wakuu wa Mikoa ni lazima wahakikishe bidhaa kama saruji, nondo,
marumaru, mabati zinavyotumika katika ujenzi ziwe vimezalishwa na
viwanda vya ndani kwa sababu vina viwango vya ubora unaotakiwa na pia
itasaidia kuondoa tatizo la soko la bidhaa hizo.
Naye,Waziri
Mwijage amewataka watendaji wanaohusika na masuala ya viwanda kutoweka
vikwazo kwa wawekezaji ambao wanakwenda katika ofisi zao kwa ajili ya
kutafuta maeneo ya kuwekeza kwenye viwanda au wanaohitaji vibali kwani
jambo hilo halina tija.
mPEKUZI.
Comments