Uturuki kukiunga mkono SUZA.

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Idris Rai ameipokea kwa mikono miwili hatua ya serikali ya Uturuki, kutaka kukiunga mkono Chuo hicho kwa kuanzisha masomo ya utibabu wa meno ‘dental’.
Prof. Rai alieleza hayo kwenye mazungumzo baina yake na ujumbe wa serikali ya Uturuki ulioongozwa na balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, Ali Davutoğlu, huko katika kampasi ya SUZA, iliyopo Vuga mjini Zanzibar.
Makamu huyo mkuu wa SUZA, alisema kuanzishwa kwa kitivo cha masomo ya utibibu wa meno, kutaisaidia Zanzibar kupata wataalamu wazalendo watakao hudumia wananchi wanaokabiliwa na matatizo ya afya ya meno.
Katika hatua nyengine, Prof. Rai alimuomba balozi huyo aangalie maeneo mengine ambayo taasisi za elimu ya juu nchini Uturuki inaweza kushirikiana na chuo hicho.
Alisema SUZA kipo tayari na kimefungua mlango wake kwa taasisi za elimu nchini Uturuki hasa kwa kupatia nafasi za masomo kwa wakufunzi wa kada mbalimbali wa SUZA.
Sambamba na hilo, Prof. Rai alipendekeza uwepo ushirikiano na taasisi za elimu ya juu za nchini Uturuki kwenye eneo la ufanyaji wa utafiti pamoja na machapisho mbalimbali ya kitaaluma.
Kwa upande wake, balozi Ali Davutoğlu, alisema kupitia shirika la ushirikiano la kituruki (TIKA), atahakikisha maafikiano yaliyofikiwa yatafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
Alisema suala la kuazishwa kitivo cha afya ya meno ni jambo la muhimu na kwamba kitaanzishwa chini ya ushirikiano na SUZA.
“Tunaheshimu kila ambalo tumelizungumza na zaidi suala la kuanzishwa kitivo cha taaluma ya afya ya meno”, alisema balozi huyo.
Alisema Uturuki inao wataalamu wa kutosha wanaoweza kuja SUZA kutoa mafunzo hayo kwa wataalamu wa afya wa Zanzibar.
Zanzibarleo.

Comments