Naibu
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Elias John Kwandikwa amewataka wakazi wa
mikoa ya Mwanza na Geita kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii
zitakazojitokeza wakati wa ujenzi wa daraja litakalounganisha eneo la
Kigongo na Busisi Mkoani Mwanza.
Amesema
maandalizi kwaajili ya ujenzi wa daraja hilo la aina yake hapa nchini
yako katika hatua ya usanifu wa kina hivyo ujenzi wake utaanza mara
baada ya mkandarasi wake kutangazwa na linatarajiwa kuwa na urefu wa
kilomita 3.2, litakapokamilika.
“Hakikisheni
mnatoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi ya ujenzi iwe nyepesi na
wale watakaopata fursa za ajira fanyeni kazi kwa weledi, bidii na
nidhamu” amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Amesema
Serikali inatumia fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ya muda mrefu
hivyo ni jukumu la wananchi kujiandaa na kubaini fursa za kiuchumi na
kijamii na kuzitumia.
Naye
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza Mhandisi Marwa
Rubirya amesema daraja hilo litakuwa na njia nne za kupitisha magari,
njia ya waenda kwa miguu ambapo pia litakuwa na kina kitakachoruhusu
meli kupita chini ya daraja hilo.
Mhandisi
Rubirya amesisitiza umuhimu wa wananchi wenye maeneo yatakayotumika
kupisha ujenzi huo kutoa ushirikiano ili kuharakisha kazi hiyo.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua kivuko cha
Kigongo-Busisi na kuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA),
kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi kuhusu usalama na matumizi
sahihi ya utumiaji wa vivuko.
Amezungumzia
umuhimu wa TEMESA kuweka mifumo ya kielektoniki ili kuwezesha waendesha
vivuko, wakusanya mapato na wasimamizi kuwa na mawasiliano ya pamoja na
hivyo kuwezesha vivuko kuwa na abiria na mizigo inayokubalika wakati
wote.
Mkuu
wa kivuko cha Kigongo –Busisi Mhandisi Abdala Atiki amesema kivuko
hicho kwa sasa kinahudumiwa na Mv- Mwanza na Mv- Misungwi ambapo zaidi
ya abiria elfu sita na mia tano huvushwa kwa siku.
Zaidi ya mikoa 12 nchini ina maeneo yenye mahitaji ya vivuko ambapo takriban vivuko 30 vinatoa huduma nchini kote.
Mpekuzi.
Comments