Tatizo la uhaba wa mchele kumalizwa – Amina.

Image result for balozi amina salum aliWAZIRI wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali, amesema kuadimika kwa mchele katia soko la dunia ni miongoni mwa sababu zilizosababisha kupanda kwa bei mchele Zanzibar.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, waziri huyo alisema hali hiyo imesababishwa kuchelewa kwa mavuno ya mchele nchini Pakistan, ambapo mchele unaongizwa nchini ndiko unakoagizwa kwa wingi.
Alisema kwa kawaida mavuno ya mchele huanza Septemba kila mwaka.
Alisema kwa mwaka huu, mavuno ya mchele nchini Pakistan yamechelewa na yameanza Oktoba ambapo mchele uliokuwepo katika kipindi cha Septemba katika soko la dunia haukuwa na mazingira mazuri hali ambayo imesababisha wafanyabiashara wa Zanzibar kutoagiza mchele huo.
Sababu nyengine alisema ni upatikanaji wa usafiri ambapo kwa kawaida meli za vyakula vya Zanzibar huwa haziji moja kwa moja na huishia mjini Mombasa, Kenya.
“Hali hii inatokana na changamoto ya bandari yetu ambayo ni ndogo na kuchelewesha ushushaji wa mizigo kwa wakati na matokeo yake huwa tunasubiri meli nyengine kutoka Zanzibar kwenda Mombasa kuchukua mizigo hiyo”, alisema.
Aidha alisema matarajio ya upatikanaji wa mchele na kushuka kwa bei tayari yapo vizuri kwani wafanyabishara wakubwa wanaoagiza mchele wameagiza mchele mpya ‘new crop’ kutoka Pakistan ambapo idadi kontena 200 sawa na wastani wa tani 5,400 zinatarajiwa kuingia nchini.
Akizungumzia bei, alisema inatarajiwa kushuka na kufikia kati ya shilingi 58,000 hadi 62,000 kwa polo la kilo 50 kama ilivyokuwa awali ambapo bei ya reja reja itakuwa shilingi 1,300 kwa kilo.
Zanzibarleo.

Comments