Somalia kugeuka kuwa uwanja wa migogoro ya magaidi wa Daesh na ash-Shabab.

Somalia kugeuka kuwa uwanja wa migogoro ya magaidi wa Daesh na ash-ShababTawi la kigaidi la genge la Daesh (ISIS) nchini Somalia, limewaonya wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab lenye mfungamano na genge la al-Qaidah, kuhusiana na ukwamishaji mambo wowote katika kutekeleza operesheni zake nchini humo.

Kundi hilo la al-Somal al-Jadid, tawi la Daesh nchini Somalia sambamba na kuashiria kwamba genge la ash-Shabab limekuwa likikwamisha harakati za wanachama wake, limedai kwamba wakati wa kulipiza kisasi kwa wanachama hao wa ash-Shabab umefika. 

Vitisho vya kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) vimetolewa katika hali ambayo wiki iliyopita kundi la kigaidi la ash-Shabab, lilimuua mwanachama wake mmoja katika eneo la Jubba, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wakati alipokuwa anakusudia kujiunga na genge la Daesh. 

Mbali na tukio hilo magaidi hao wa ash-Shabab waliwatia mbaroni watu wengine kadhaa katika tukio hilo.
 
Kundi la Daesh lililopiga kambi katika miinuko ya kaskazini mashariki mwa Somalia, linafanya juhudi za kujipenyeza zaidi ndani ya nchi hiyo, hata hivyo kundi la ash-Shabab sambamba na kulizuia kundi hilo, limewaua wanachama wake kadhaa. 

Mwaka 2011, wanachama wa kundi la ash-Shabab walitimuliwa kutoka mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, pamoja na hali hiyo wamekuwa wakidhibiti sehemu pana ya nchi hiyo. 

Makundi hayo ya kigaidi ambayo yote yanafuata idolojia ya Kiwahabi, yameingia katika vita baina yao, katika hali ambayo mwaka 2015 kulienea habari kwamba kundi la ash-Shabab lilikuwa limetoa kiapo chake cha utiifu kwa kundi la Daesh (ISIS).

 parstoday

Comments