Lugola azipongeza taasisi za wizara yake.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Alphaxard Lugola amesema ameridhishwa na utendaji wa taasisi zilizopo katika wizara yake kwa upande wa Zanzibar, kwani zinatekeleza vyema majukumu yao.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi kwa taasisi zikizopo chini ya wizara hiyo yenye lengo la kuangalia utendaji wa kazi kwa wafanyakazi wa taasisi hizo.

Alisema, katika taarifa zao zimemridhisha kuamini kuwa wamekuwa wakifanya kazi ikiwemo kwa jeshi la polisi ambalo limeweza kudhibiti uhalifu visiwani Zanzibar.

Alisema kwa mujibu wa ripoti, uhalifu unaendelea kupungua na kudhibitiwa kwani ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba mwaka huu, ripoti ya uhalifu kwa vitendo vya uhalifu umepungua kwa asilimia 34 pamoja na makosa madogo yapo kwa asilimia wamepunguza na kudhibiti kwa asilimia 57.

Aidha alisema takwimu hizo zinaonesha kuwa Zanzibar kumekuwepo kwa mafanikio ambayo yamekuwa yakiendelea kupatikana katika kudumisha amani, utulivu na usalama.

Hivyo, alimpongeza Kamishna wa Jeshi la polisi Zanzibar na watendaji wake kwa kazi nzuri anayoifanya licha ya kuwepo kwa changamoto zinazomkabili.

Akizungumzia taasisi ya Nida, alisema kuwa wamekuwa wakifanyakazi nzuri na kufanikiwa malengo waliyojiwekea na kufanikiwa kwa asilimia 99 pamoja na kuweza kutoa vitambulisho hivyo kwa asilimia 90.

Kwa upande wa Uhamiaji, alisema kuwa wameweza kuendelea kudhibiti wa uingiaji, utokaji na ukaazi wa wageni na kuweza kukamata wahamiaji haramu, kufikishwa mahakamani na wengine kurudishwa walikotoka.

“Kwa kweli ni jambo la kupongezwa sana kwa watendaji wa taasisi hizi mmeonesha moyo wa kufanyakazi, kwani hata uhalifu umepungua kwa asilimia kubwa zaidi na upatikanaji wa huduma kupitia taasisi zenu zimekuwa umeimarika”, alisema.

Hivyo aliwathibitishia wananchi kwamba wizara yake itaendelea kudumisha amani, usalama na utulivu uliokuwepo sambamba na kuendeleza ulinzi wa kudumu visiwani kupitia vyombo vya ulinzi vilivyopo chini ya wizara hiyo.

Zanzibarleo.

Comments