RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amezipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Idara za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha Zanzibar inaedelea kuwa salama.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Kangi Alphaxard Lugola uliofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais ambapo viongozi wengine waliofutana na Waziri Lugola ni Meja Jenerali Jacob Gideon Kingu, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Kailima Ramadhan.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Zanzibar iko salama hali ambayo imeweza kuwapelekea wananchi wake waendelee kuishi kwa amani na utulivu mkubwa.
Rais Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo inatokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na vikosi vyote vya Idara zilizomo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi likiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji pamoja na Idara ya Vitambulisho vya Taifa.
Alieleza kuwa kupungua kwa vitendo vya uhalifu kwa asilimi 34 pamoja na makosa madogo kwa asilimi 57 kwa kipindi cha Januatri hadi Oktoba mwaka huu, kumeonesha wazi kuwa mafanikio makubwa yanaendelea kupatikana katika kudumisha amani, utulivu na usalama hapa Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa kazi imefanywa vizuri sana hadi kufikia hatua hiyo ya mafanikio na kueleza imani yake kubwa aliyonayo kutokana na uongozi wa Wizara hiyo ambao umeanza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Dk. Shein aliueleza uongozi huo juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilizozichukua katika kuhakikisha vitendo vyote vinavyohatarisha amani na usalama vinadhibitiwa ipasavyo kwa kuandaa mikakati maalum ili wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea Zanzibar wakiwemo watalii wanakuwa salama kwa kuweka vifaa maalum vya kisasa vya ulinzi.
Rais Dk. Shein alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba sifa njema ya Zanzibar kuwa ni sehemu salama yenye utulivu inabakia na inakuwa ya kudumu na inaendelea kuwa ni kichocheo cha kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi katika nyanja zote ikiwemo sekta ya utalii.
Mapema Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Alphaxard Lugola alimueleza Rais Dk. Shein mikakati maalum iliyowekwa na Wizara yake katika kuhakikisha ulinzi, amani na usalama inakuwa ya kudumu hapa Zanzibar.
Comments