Alisema hayo jana ikulu mjini Zanzibar wakati akizungumza na Makamu
Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, Cai Defeng, aliepo
nchini Tanzania kwa ziara ya siku sita kufuatia mwaliko wa Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.
Dk. Shein alitoa shukurani kwa China kwa kuendelea kuiunga mkono
Zanzbar katika kuendeleza miradi ya maendeleo ambayo ni chachu katika
kukuza uchumi wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Jamhuri ya
Watu wa China ambapo ujio wa kiongozi huyo unathibitisha ukweli huo.
Alisema China na Zanzibar zina historia kubwa tangu wakati wa
kupigania uhuru hadi leo, ambapo nchi hiyo ilikuwa ya mwanzo kuyatambua
mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
Zanzibar alipongeza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya CCM na
Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) chini ya uongozi wa Rais, Xi
Jinping.
Alizipongeza hatua za China kuunga mkono jitihada za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo
afya, elimu, kilimo, maji safi na salama, miundombinu, viwanda na
mengineyo.
Dk. Shein alipongeza juhudi zinazochukuliwa na nchi hiyo katika kutoa
nafasi za masomo kwa wanafunzi kutoka Zanzibar sambamba na ushirikiano
uliopo kutoka jimbo la Jangsu katika kuimarisha sekta ya afya.
Alipongeza azma ya China kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano
katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo uchumi wa bahari, uvuvi,
uwekezaji pamoja na gesi asilia na mafuta.
Aliwakaribisha wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza Zanzibar
sambamba na watalii wa nchi hiyo kuitembelea Zanzibar kutokana na
vivutio kadhaa vilivyopo nchini.
Alieleza kuwa uchumi wa bahari ni miongoni mwa mambo muhimu yaliopewa
kipaumbelea na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uchumi
wake hasa ikizingatiwa kuwa ni mwanachama wa nchi zinazopakana na
bahari ya Hindi (IORA).
Pia, alipongeza ushirikiano uliopo kati ya Bunge la Jamhuri ya Watu
wa China na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar.
Katika maelezo yake, Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kwa kumualika
kiongozi huyo kuitembelea Tanzania.
Aidha, alimuhamikikishia kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaendelea kuthamini juhudi za Jamhuri ya watu wa China chini
ya kiongozi wake Rais, Xi Jinping, kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Alieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe
Magufuli, ataendeleza uhusiano uliopo kati ya nchini mbili hizo kwa
kutambua ushirikiano wa kihistoria ambao umeanzishwa na waasisi wa
Mataifa hayo.
Nae, Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, Cai
Defeng alimuhakikishia Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo kwa lengo la kukuza
uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.
Alisema China iko tayari kuisaidia Zanzibar katika kuendeleza uchumi
wa bahari, uvuvi, utalii na sekta nyengine huku akiahidi kuimarisha
sekta ya uwekezaji Zanzibar kwa kuwaalika wawekezaji wa China kuja
kuwekeza Zanzibar.
Aidha, alipongeza mazungumzo aliyoyafanya na viongozi wa mabunge
nchini pamoja na kueleza ushirikiano mzuri uliopo kati ya bunge la nchi
yake na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar.
Alipongeza mapokezi aliyoyapata pamoja na ukarimu wa wananachi na
viongozi wa Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
jumla.
Zanzibarleo.
Comments