Dk. Shein afungua mkutano baraza la biashara.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein amesema kuanzishwa kwa sheria namba 10 ya mwaka 2017 ya Baraza la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZNBC) kutaimarisha biashara na kukuza uchumi nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo jana ikulu mjini Zanzibar wakati akifungua mkutano wa pili wa baraza la taifa la biashara la Zanzibar (ZNBC) wa siku moja ambao pia, mbali ya mambo mengine ulijadili maandalizi ya jukwaa la tisa la biashara la Zanzibar litakalofanyika Novemba 24, 2018.

Dk. Shein alieleza imani yake kubwa kuwa sheria hiyo ya mwaka 2017 italeta kasi kubwa katika  kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali kwa lengo la  kukuza uchumi.

Alisema mkutano huo umejadili mambo yenye mnasaba na jukwaa la tisa la Biashara la Zanzibar ambao utaweza kusaidia katika kulifanikisha Baraza la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZNBC) ili kufikia malengo  iliyojiwekea.

Alisisitiza haja kwa wajumbe wa baraza hilo kuhudhuria vikao ipasavyo kutokana na umuhimu mkubwa wa baraza hilo kwani vikao hivyo huamua na kujadili mambo muhimu.

Alisisitiza haja ya kuandaliwa taratibu maalum za kuwasaidia vijana ili waweze kushiriki vyema katika uzalishaji wa bidhaa zikiwemo za kilimo, uvuvi, utalii na nyenginezo ambapo kwa upande wa Serikali alieleza hatua zinazochukuliwa ili kufanikisha hilo.

Dk. Shein alisema kuna haja ya sekta binafsi kushirikiana na sekta ya umma katika kuwasaidia vijana huku akisisitiza kuwa vikao hivyo vina umuhimu mkubwa katika kujenga muktadha mzuri wa malengo yaliokusudiwa.

Akitoa maelezo juu ya sheria namba 10 ya 2017 ya Baraza la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZNBC) Mohammed Khamis, Mwanasheria kutoka Wizara ya Biashara na Viwanda alisema kuwa kuwepo kwa sheria hiyo kuna umuhimu mkubwa katika kuimarisha sekta ya  biashara na uchumi.

Alisema kuwa sheria hiyo imeeleza mambo mengi ikiwa pamoja na muundo wa vyombo mbali mbali, likiwemo Baraza la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZNBC), malengo kadhaa pamoja na kazi mbali mbali za Baraza la Taifa la Zanzibar.

Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alieleza haja kwa wamiliki wa hoteli, kuwalipa kwa wakati vijana wanaojiajiri ambao huuza  bidhaa zao zikiwemo za kilimo kwa ajili ya matumizi katika hoteli hizo.

Nae Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali alieleza umuhimu wa mashirikiano kati ya sekta Binafsi na Serikali pamoja na kuitaka sekta Binafsi kuwainua wafanyabiashara wadogo wadogo.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Zanzibar, Bakari Ally Bakari alieleza kuwa kauli mbiu ya Jukwaa la Biashara la 9 la Zanzibar mwaka huu ambalo linatarajiwa kufanyika Novemba 24, 2018 kuwa ni “Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kukuza ajira kwa vijana”.

Zanzibarleo.

Comments