ZEC, vyama vyasaini makubaliano uchaguzi Jang’ombe.

TUME ya Uchaguzi Zanzibar, imetiliana saini ya makubaliano ya muongozo wa maadili ya vyama vya siasa na wajumbe wa kamati maalum ya uchaguzi mdogo wa jmbo ja Jang’ombe.
Hayo yalifanyika katika ukumbi wa tume, Maisara mjini Unguja.
Wajumbe hao walikutana katika kikao hicho kwa ajili ya kusaini muongozo huo ambao una lengo la kuweka utaratibu mzuri wa kuendesha uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji Khamis Ramadhan Abdallah, aliwaomba wagombea kushirikiana katika kutekeleza maadili hayo.
Akisoma muongozo huo Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Mbarak Said, alisema, tume itahakikisha inatoa huduma na nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa bila ya upendeleo.
Aidha alisema, kupitia vyombo vya usalama, serikali inasimamia usalama wa nchi na kutoa ulinzi unaostahiki katika mkutano na kampeni pamoja na mikusanyiko yote iliyo rasmi ya vyama vya siasa.
Alisema, vyama vya siasa vitashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika usimamizi wa sheria na kudumisha amani wakati wa kampeni, upigaji kura, utangazji wa matokeo na baada ya matokeo.
Naye Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Jang’ombe, Mwanapili Khamis Mohammed, aliwataka wagombea kumaliza mapema kampeni zao katika muda uliopangwa ambao ni saa 12 jioni.
Zanzibarleo.

Comments