Wizara yasikia kilio cha wananchi Mtambile-Kengeja.

WANANCHI wanaotumia barabara ya Mtambile-Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, wameanza kupata faraja kufuatia barabara hiyo, kuanza kuzibwa mashimo kwa kutumia lami, kazi inayofanywa na mafundi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.

Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia watendaji mafundi wa wizara hiyo, wakiwa na vifaa vyao wakianza kazi ya kuziba viraka kwenye mtaa wa Mtambile kueleka Kengeja.

Wiki tatu zilizopita, gazeti la Zanzibar Leo kwenye ukurasa wake wa mbele lilieleza tabu wanayoipata wananchi wanaotumia barabara hiyo, kutikana na kuwepo mashimo yenye kina kirefu.

Baadhi ya wananchi wanaotumia barabara hiyo, walisema uamuzi wa wizara hiyo ni mzuri na unafaa kuungwa mkono.

Mmoja ya wananchi hao, Asha Makame Ussi wa Mwambe, alisema barabara hiyo ilikuwa imeharibika kwa kiwango kikubwa na kitendo cha kutiwa viraka ni faraja kwao.

Alisema wamekuwa wakipata usumbufu wa kusafiri wao na mazao yao, kutokana na kuharibika vibaya barabara hiyo.

Nae Mwashamba Ramadhan Hamdan, alisema sasa itakuwa rahisi hasa pale mama wajawazito wanapokimbilia hospitali kujifungua.

“Ilikuwa ni dhiki na shida isio na mwisho kwa barabara yetu hasa pale anapotokea mzazi anataka kwenda hospitali ya Mkoa ya Mkoani, mashimo yalikuwa ni mengi tena makubwa”, alieleza.

Nae mfanyabishara, Mohamed Issa Nassor, alisema barabara inapokuwa nzuri huwapa urahisi wa kusafirisha bidhaa zao kwa bei nafuu.

Zanzibarleo.

Comments