Akifunga mafunzo ya siku mbili ya kuhamasisha matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa wajumbe wa baraza hilo, Chukwani, alisema kufanya hivyo kutasaidia wananchi kuhamasika katika kupanga uzazi kwa maendeleo ya nchi na afya zao.
Aidha alisema wananchi wa Zanzibar wana kila sababu ya kupanga uzazi ili kusaidia kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
“Wenzetu China walijipangia kuwa kila mwananchi azae mtoto mmoja na wameweza, iweje na sisi tusijipangie,” alisema.
Aliwaomba wajumbe hao kutilia mkazo zaidi matumizi ya uzazi wa mpangilio kwa kina baba kwani ushiriki wao ni mdogo katika huduma za uzazi hali inayopelekea kina mama wengi kushindwa kutumia uzazi huo.
Nao wajumbe wa baraza hilo, wakichangia mada juu ya njia ya uzazi wa mpango, waliowamba wananchi kuondoa dhana potofu kuwa dawa za uzazi wa mpango zinasababisha madhara yakiwemo ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi.
Walisema kupitia tafiti za kisayansi zilizofanywa, njia hizo hazina madhara yoyote badala yake zina faida katika makuzi ya mtoto na kuimarisha afya ya mama.
Hata hivyo, waliishauri wizara ya afya kutafuta njia ya kulisomesha somo hilo maskuli ili wananchi wapate uelewa zaidi juu ya hasara na faida zinazojitokeza.
Mafunzo hayo, yaliandaliwa na Wizara ya Afya kupitia kitengo shirikishi ya afya ya mama na mtoto kwa kushirikiana na Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA).
Zanzibarleo.
Comments