Uwanja wa kisasa waanza kujengwa Micheweni.

KAMPUNI ya Ujenzi ya Kin Investment LTD ya Chake Chake, imekabidhiwa ujenzi wa uwanja wa michezo Kishindeni wilaya ya Micheweni Pemba.
Uwanja huo utakaokuwa na viwanja vya mbalimbali, utaweza kuhamasisha vuguvugu la kuibua vipaji vya wachezaji kutoka wilaya ya Micheweni na Wete ndani ya mkoa huo wa Kaskazini Pemba
Hafla hiyo ya makabidhiano kwa wakandarasi wa ujenzi huo, ilifanyika huko katika uwanja wa Kashindeni na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikali, kamati ya ulinzi na usalama na viongozi wa CCM Mkoa huo.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, alisema, kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kuibua vipaji vya wachezaji mbali mbali, pamoja na kuendeleza michezo kwa katika wilaya hiyo.
“Kukamilika kwa uwanja huo ni dhahiri michezo mbali mbali sasa itaanza kukua ikiwemo riadha, kikapu”, alisema.
Aidha, aliwataka Wanamicheweni kuhakikisha wanakuwa wasimamizi na walinzi wa mali za uwanja huo, ili uweze kukamilika kwa wakati sambamba na wakandarasi kujenga kwa kiwango cha hali ya juu.
“Sasa tunataka kuona timu za Micheweni nazo zinawika katika Ligi Kuu ya Zanzibar, sio kila siku Jamhuri na Mwenge”, alieleza.
Kamishna wa Michezo Zanzibar, Sharifa Khamis, alisema, kujengwa kwa kiwanja hicho ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohames  Shein ambapo uwanja wa Kishindeni utakuwa wa pili kujengwa kati ya viwanja vitano vya Zanzibar, alivyoviahidi kupitia Ilani ya CCM 2015/2020.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni, Salama Mbarouk Khatib, alimpongeza, Dk. Shein kwa uamuzi wake wa kuamua kujengwa uwanja katika wilaya hiyo, huku akiahidi kushirikiana na wakandarasi ili uweze kukamilika kwa wakati.

Naye Ofisa Mdhamini Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba, Fatma Hamad Rajab, aliwataka vijana kujiandaa kwa mashindano mbali mbali baada ya kukamilika kwa uwanja huo.

Mkandarasi wa ujenzi huo, Issa Bilal,  aliahidi kuujenga uwanja huo kwa kiwango cha kisasa zaidi, huku akitarajia kazi hiyo kukamilika ndani ya miezi mitatu.


Zanzibarleo.

Comments