Jana wakati boti ya kwanza ya Kilimanjaro ikijiandaa kuondoka Zanzibar kuelekea Dar es Salaam saa 1:00 asubuhi na abiria wakiwa tayari kupanda boti hiyo, baada ya kukaa kwa muda wakisubiri, taarifa ilitolewa kwamba huduma ya usafiri imesitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa iliyosababishwa na upepo.
Baada ya taarifa hiyo, wasafiri waliokuwepo katika bandari ya Malindi waliondoka huku wengine wakilalamikia kutopewa taarifa mapema ili kutafuta huduma nyengine ya usafiri.
“Tulipata taarifa tukiwa hapa, mimi nilikuwa naunganisha na safari nyengine sasa imeathirika,” alisema mmoja ya wasafiri aliejitambulisha kwa jila na Ali Issa.
Kampuni ya Azam Marine na Kilimanjaro Fast Ferries kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (ZMA) ilithibitisha kusitisha safari za Dar es Salaam mpaka ZMA itakapotoa tangazo la kuruhusu safari hizo.
Mbali ya usafiri wa boti kuathirika, shughuli za uvuvi pia zimeathirika kwa kiasi kikubwa ambapo hakuna chombo chochote cha uvuvi kilichokwenda baharini.
Uchunguzi umebaini hali hiyo imesababisha kuadimika kwa samaki katika masoko ya Malindi na Darajani na wale wachache walioonekana waliuzwa kwa bei ya juu.
Kwa muda wa siku tatu sasa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kanda ya Zanzibar, iliwataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na upepo mkali unaovuma baharini wenye kusababisha mawimbi makali.
Zanzibarleo.
Comments