Ujenzi wa Terminal 3 Katika Uwanja wa Ndege JNIA Kugharimu Bilioni 560.....Utakuwa na Uwezo wa Kupokea Ndege 19 kubwa na Ndogo 11 Kwa Mpigo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe, alifanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo na hatua iliyofikiwa katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Uwanja huo una historia ndefu. Ulianzia katika kipindi kirefu miaka 62 iliyopita katika zama kabla ya uhuru wa Tanganyika, ikiitwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.
Baadaye
lilijengwa jengo jipya la kisasa zaidi, ambalo baadaye likaitwa
‘Terminal Two’ wastani wa miongo mitatu na nusu iliyopita, kazi
iliyoendana na upanuzi wa njia na mahitaji mengine ya uwanjani, kukidhi
maboresho ya vigezo vya kimataifa nchini.
Baadaye,
ikiwa ni kutambua mchango wa Rais wa Kwanza, Hayati Julius Nyerere,
mageuzi na maboresho ya uwanja huo yanayoendelea kulingana na kukua
mahitaji ya wateja wake, uwanja huo ulipewa jina lake.
Hivi
sasa kuna mwendelezo wa awamu nyingine, sasa kuna mradi mkubwa wa
ujenzi wa uwanja huo unaoelekea ukingoni kwa miaka mitano hivi sasa na
kuongeza kipande kingine cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere ‘Terminal Three.’
Ujenzi huo ambao hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 560, ulianza mwezi Juni mwaka 2013 na unatarajiwa kukamilika mwakani mwezi Mei na hadi sasa umekamilika kwa asilimia 82.
Akizungumza
uwanjani hapo, Mwambe anaeleza kuwa uwanja huo utatokea fursa za
uwekezaji, ikiwamo kujitokeza kwa kampuni mpya za ndege kuanza kutua
Tanzania.
“Kampuni
za ndege zikiongezeka maana yake kutakuwa na ushindani kwenye soko,
hivyo itasaidia kupunguza gharama za usafiri wa ndege kwa wananchi.
Ushindani huu ukiwapo maana yake abiria atachagua asafiri na aina ya
shirika la ndege,” anaeleza.
Mwonekano
wa uwanja huo mpya unabebwa na jengo lenye ghorofa tatu, ambayo ya
kwanza itatumika kwa ajili ya wasafiri wanaofika, ghorofa ya pili ni kwa
wasafiri wanaoondoka na ya tatu ni kwa ajili ya masuala ya utawala.
Mwambe
anasema kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo, utasaidia kuongeza tija
kwenye uwekezaji, ambayo ni eneo analolisimamia kupitia TIC.
“Ni
ukweli usiopingika kwamba, duniani nchi zenye miundombinu bora kama
viwanja vya ndege vya kimataifa, barabara, bandari ndizo zinazopata
wawekezaji wengi.
“Tumeshuhudia
kupitia serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli, maeneo
haya niliyotaja amekuwa akiyapa kipaumbele ili kuhakikisha Tanzania
ijayo inakuwa yenye uwekezaji mkubwa,” anasema.
Mwambe
anasema, wiki iliyopita Watanzania walishuhudia Rais Dk. Magufuli
alipozindua Barabara ya Juu ya Mfugale, iliyopo katika makutano ya
Barabara ya Julius Nyerere kutoka Uwanja wa Ndege kuelekea mjini na ile
ya Mandela, kutoka Ubungo kwenda Bandarini.
Pia,
Mwambe anafafanua kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge)
unaendelea na taratibu za kuanza kwa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme
nchini ‘Stiegler's Gorge’ zinaendelea.
“Kwetu
TIC maboresho haya ni faraja, kwani yatachagiza uwepo wa mazingira bora
ya biashara na uwekezaji na kuwezesha kuunga mkono juhudi zetu za
kuvutia na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza nchini,” anaeleza.
Mwambe
anataja maeneo mengine ya uwekezaji ya wawekezaji wazawa wanakoshauriwa
kuyachangamkia ni ya uendeshaji wa biashara ya magari madogo, maegesho,
maduka, hoteli na maduka ya mvinyo.
Anasema
matarajio ya serikali kwenye uwekezaji huo, ni kuhakikisha unatoa
huduma nzuri kwa wadau wakiwamo watalii, wafanyabiashara na wawekezaji.
“Kuhakikisha
unavutia zaidi wawekezaji, inatengeneza ajira kwa Watanzania, kodi
inakusanywa kwa ajili ya kuendesha huduma za jamii na kuinua hali ya
Watanzania na uchumi wa taifa,” anasema na kuongeza:
Mwambe anaishukuru serikali kujikita katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ambayo itakayoleta mapinduzi ya ukuaji uchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania (TAA), Richard Mayongela, anasema kuwa uwanja huo utakapokamilika, utaondoa msongamano wa abiria wanaotumia sehemu ya ‘Terminal Two.’
“Terminal
Two ilijengwa miaka 34 iliyopita, kwa lengo la kuboresha huduma za
usafiri zilizokuwa zikitolewa na ‘Terminal One’ iliyojengwa mwaka 1956
na ilikuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 tu kwa mwaka,” anasema.
Anabainisha
kuwa ‘Terminal Two’ ilijengwa kuwahudumia abiria milioni moja na nusu,
lakini kwa sasa inahudumia hadi milioni 2.5 kwa mwaka.
“Idadi
hii ni kubwa na imetokana na ongezeko la abiria na shughuli nyingine za
usafirishaji, jambo ambalo linasababisha changamoto katika sekta ya
anga kubaki palepale, ikiwamo kukosa ufanisi katika kutoa huduma bora
kwa wadau na mahitaji yao kwa ujumla,” anasema.
Mayongela
anafafanua kwamba, kuna dira ya kukamilika upanuzi huo wa uwanja
kutaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo nchini katika sekta
ya anga na kutaongeza safari za ndege nyingi, kutua Tanzania.
“Mashirika
ya ndege duniani yakiongezeka hapa, kutaongeza mapato kwa serikali na
vilevile kutawezesha kuitangaza Tanzania kimataifa,” anasema na
kuongeza:
“Ujenzi
wa uwanja huu, ni mkombozi mkubwa wa Watanzania katika kuboresha sekta
ya anga. Uwanja wa ndege tunaoutumia sasa, ulijengwa mwaka 1984. Hivyo,
ni miaka 34 iliyopita,” anasema.
Anafafanua
zaidi: “Kwa hiyo, utaona ni jinsi gani tunatoa huduma za usafiri wa
anga kwa sasa, kwa miundombinu iliyokuwa imelenga kuhudumia abiria
wachache wa kipindi cha miaka ya 1980.”
Kama
alivyo bosi wa TIC, Mayongela anaishukuru serikali kwa maamuzi ya
kuupanua uwanja huo, kwani umefanyika kwa wakati muafaka ukiendana na
ukuaji uchumi na maendeleo ya nchi.
Mkurugenzi
huyo anabainisha kuwa ‘Terminal Three’ itakapokamilika, itaruhusu ndege
kubwa (Dream liner 8) kupakia na kushusha abiria na mizigo yao kwa
wakati mmoja, wakati huo huo ndege tatu zikiwa kwenye eneo la maegesho.
“Kwa
namna upanuzi huu ulivyofanyika, utawezesha kuhudumia ndege kubwa za
kawaida zipatazo 19 na ndege ndogo 11 zinazoingia na kutoka nchini kwa
wakati mmoja,” anasema.
Ziara
hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, imefanyika kutokana na kituo hicho
cha uwekezaji kuwa mdau mkubwa wa uwekezaji, pia kubadilishana mawazo,
uzoefu na kushauriana na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, kuhusu uwanja huo wa
ndege.
Mayongela
anasema, lengo lao ni kuhakikisha uwekezaji huo unavutia na kuchochea
wawekezaji kuja zaidi Tanzania na kuirudishia faida serikali, Watanzania
na taifa kwa jumla.
Mpekuzi.
Comments