Shein azindua mradi ulinzi wa mji salama.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema katika kuhakikisha vitendo vinavyohatarisha amani vinadhibitiwa, serikali imeaandaa mikakati ili wananchi na wageni wanaoitembelea Zanzibar wanakuwa salama.
Alieleza hayo jana katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa ulinzi wa mji salama, hafla iliyofanyika ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni mjini Unguja, ambapo kabla ya hapo alizindua kituo cha mfumo wa kuimarisha usalama kilicho Maisara.
Akiwa Maisara, alipata maelezo juu ya uendeshaji wa kituo hicho na jinsi vifaa vinavyofanya kazi ikiwemo gari maalum za kuangalia usalama, pikipiki na matumizi ya ‘drone camera’.
Dk. Shein alisema lengo la serikali ni kuhakikisha sifa njema ya Zanzibar kuwa ni sehemu salama yenye utulivu inabakia na inakuwa ya kudumu na inaendelea kuwa ni kichocheo cha kuongeza kasi ya maendeleo.
Alisema serikali kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inabuni mikakati na kuvitumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha nchi na watu wako salama.
Alieleza kuwa serikali imeamua kuweka vifaa vya kisasa vya ulinzi kwa lengo la kuimarisha hali ya usalama katika mji wa Zanzibar, kwani vifaa hivyo vina uwezo wa kuwabaini wahusika wa matukio kwa haraka na ufanisi.
Aliwahimiza wananchi kuvitumia vyema vifaa hivyo na wavitunze ili viweze kutumika kwa muda mrefu na wote wawe walinzi wa nchi yao huku akisisitiza kuwa amani, umoja na usalama hivi sasa utaimarika.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Radhia Rashid Haroub, alisema serikali iliamua kuanzisha mradi huo wa kuimarisha mfumo wa usalama hapa Zanzibar katika mwezi Aprili 2015 na kutiliana saini na kampuni ya ROM Solution Ltd.
Kuimarisha ulinzi kufikia katika kiwango cha Kimataifa, katika maeneo ya uwanja wa ndege, bandarini, Mji Mkongwe na baadhi ya barabara kuu za kuingilia katika mji wa Zanzibar uwanja wa ndege ikiwa ni pamoja na gari tatu katika viwanja vya ndege, mbili Unguja na moja Pemba
Alisema kuwa jumla ya kamera 56 zimefungwa katika eneo la uwanja wa ndege na bandarini kamera 42 katika eneo yanayozunguka bandari, boti maalum kwa ajili ya ulinzi wa baharini nazo zimeongezeka, kamera 682 zimewekwa katika Mji Mkongwe na kamera 96 zimewekwa katika barabara ambazo zina uwezo wa kubaini vyombo vya usafiri vinavyokiuka sheria, ambapo kwa ujumla kamera 877 zimefungwa katika mradi huo.
Zanzibarleo.

Comments