Shein akutana na wanafunzi bora.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanafunzi kuongeza kasi katika kusoma masomo ya sayansi na Sanaa, kwani bado nchi inahitaji wataalamu wa fani mbalimbali ili kwenda sambamba na mabadiliko ya karne ya 21.
Dk. Shein alieleza hayo jana katika hafla ya kuwapongeza na kuwazawadia wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita waliofanya vizuri katika mitihani ya taifa, ambapo alipata nafasi ya kula nao chakula cha mchana, hafla iliyofanyika katika viwanja vya ikulu mjini Zanzibar.
Alisema kila nchi ina mahitaji ya wataalamu wa fani za sayansi na sanaa, wakiwemo madaktari, wahandisi, marubani, viongozi, wanasheria, wanazuoni, mashekh na fani nyengi kadhaa.
Alifahamisha kuwa serikali imetoa udhamini wa nafasi 30 kwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza kwenda kusoma vyuo vya ndani na nje ya Zanzibar.
Dk. Shein alisema serikali inathamini juhudi za wanafunzi hao katika kutafuta elimu na ndio kila mwaka amekuwa akiongeza nafasi za udhamini kwa wanafunzi wanaopata daraja la kwanza.
“Nilianza na wanafunzi 10 wa daraja la kwanza kidato cha sita, baadae wanafunzi 15 na sasa serikali imeongeza hadi wanafunzi 30 waliopata daraja la kwanza”, alisema.
Alieleza kufurahishwa kwake na taarifa ya wanafunzi 126 wanawake 48 na wanaume 78 wa kidato cha sita katika mwaka huu wa 2018 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza na wanafunzi wanawake 61 na wanaume 74 ambao ni jumla ya wanafunzi 135 walifanya mitihani ya Kidato cha Nne mwezi Novemba mwaka 2017 wamepata daraja la kwanza.
Aliwapongeza wanafunzi wanaume kwa kuweza kupata daraja la kwanza kwa wingi zaidi kuliko wanafunzi wanawake kutokana na mwaka jana kuwatia moyo na hamasa katika sherehe kama hizo, huku akieleza anaamini mwakani wanawake wataendelea kushika nafasi yao ya kuongoza.
Aliwapongeza wanafunzi hao wote kwa kufanya vizuri katika masomo ya sayansi, biashara na sanaa na kutoa pongezi maalum kwa Biubwa Khamis Ussi na Fahad Rashid kwa kupata daraja la kwanza la kiwango cha alama 3 kila mmoja na kuwemo katika orodha ya wanafunzi 10 bora Tanzania.
 Zanzibarleo.

Comments