Juzi, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilieleza namna udanganyifu huo ulivyofanyika na kutangaza kufuta matokeo ya shule zote za Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma na Shule ya Kondoa Integrity ya mkoani hapa.
Halmashauri hiyo ina shule za msingi 103 huku wanafunzi walioandikishwa kufanya mtihani huo wakiwa 5,362. Hata hivyo, waliofanya mtihani huo ni 5,171.
Nyingine zilizotajwa kuhusika katika udanganyifu huo ni Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za Dar es Salaam; Alliance, New Alliance na Kisiwani za Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Odunga alisema waratibu elimu kata waliovuliwa madaraka na majina ya kata zao katika mabano ni Husein Waziri (Goima) Deus Philip (Farkwa), Yona Kogwi (Paranga), Ruta Rutaigwa (Chemba) Gido Bulaya (Churuku).
Alisema walimu na shule zao katika mabano ni Noela Chambo (Farkwa) Jinjo Mohamed (Kikima) Joseph Mvula (Bugenika), Hamidu Idrisa (Chemba) na David Kilunda (Makama).
Juzi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilitengua uteuzi wa ofisa elimu wa Chemba na ofisa taaluma wa Wilaya ya Chemba na ofisa elimu msingi wa Wilaya ya Kondoa DC.
Odunga alisema Septemba 6 wakati wanafunzi wakiendelea na mitihani ya kumaliza elimu yao walipata fununu kwamba kuna dalili za udanganyifu katika Shule ya Msingi ya Farkwa.
“Kamati (ya ya mitihani)ikachukua hatua za haraka kwenda katika shule hiyo na kufanya upekuzi kwa wahusika wote waliokuwa katika lile eneo na ndipo ilipobainika kuwa kuna ujumbe kwenye simu (sms) ambazo walikuwa wakitumiana zikionyesha kuwa ni majibu ya mitihani,” alisema
Alisema uchunguzi ulianza kwa Kamati ya Mitihani ya Wilaya ya Chemba kuwasiliana na vyombo husika na kisha wakawakamata wahusika na simu zao zikakusanywa.
“Na haraka sana wakawasiliana na Kamati ya Mitihani ya Mkoa na wenyewe wakachukua hatua haraka za kufika katika eneo la tukio. Kwa hiyo kamati hizi mbili zikaanza kufanya uchunguzi wa haraka na kufuatilia zile sms zilikuwa na mahusiano gani na mtihani.”
Alisema uchunguzi uliendelea kufanywa kwa mahojiano kati ya walimu wakuu wa baadhi ya shule na wasimamizi wa mitihani ambao baadhi yao walikiri kusambaza ujumbe wa taarifa za mitihani na kubainisha kuwa Takukuru pia watachunguza mazingira ya rushwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema walimu wanne waliokuwa wasimamizi wa mitihani katika shule binafsi ya Kondoa Intergrity nao wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Kuhusu kuwajibika yeye na mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo kuhusiana na tukio hilo, Odunga alisema hajaona mahali ambako wamekosea.
“Kamati yangu imefanya kazi na vyombo vya usalama vipo ndani ya ile kamati, ubainifu wa udanganyifu umebainishwa na vyombo vyetu kwa hiyo kamati yetu imefanya kazi yake na hatua zimechukuliwa haraka. Sioni kama dhana ya uwajibikaji inakuja hapo,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alipoulizwa iwapo kuna watu wanaowashikilia kuhusiana na tukio hilo alijibu kwa kifupi kuwa yupo mkutanoni.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Dk Semistatus Mashimba alisema shule za msingi katika wilaya hiyo zipo 103 na wanafunzi walioandikishwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 5,362 lakini waliofanya mtihani uliofutwa ni 5,171.
Akitoa maoni yake, Mwalimu mstaafu, Masungu Mligo alisema tatizo hilo limetokana na baadhi ya walimu kutojali miiko ya taluma akisema katika miaka yake 40 ya ufundishaji hajawahi kuona jambo kama hilo.
Mwalimu Idrisa ambaye ni miongoni mwa waliovuliwa madaraka, alisema wanafunzi wengi baada ya kumaliza masomo yao ya darasa la saba husambaa maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo kujiandaa na masomo ya sekondari.
“Baada ya kusikia habari hizi mimi mwenyewe nilifadhaika. Kitu kama hicho hakipo, siamini kama kipo,”alisema alipoulizwa kama aliwahi kusikia kuhusu wizi huo.
Mmoja wa wanafunzi waliofutiwa mitihani katika Shule ya Msingi Chemba, Fauza Hassan alisema kuwa amejisikia vibaya baada ya kupata taarifa hizo katika vyombo vya habari.
“Mitihani ilikuwa ni migumu na tulijiandaa kwa miezi miwili kwa kukaa kambini. Tutafanya tena kwa sababu ni maamuzi ya Serikali,”alisema.
Comments