Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta,
ameshindwa kujiunga na kambi ya timu ya Taifa Stars hapa nchini, badala
yake atajiunga na timu moja kwa moja nchini Cape Verde.
Afisa
habari wa TFF Cliford Ndimbo ameweka wazi kuwa nahodha huyo atajumuika
na timu huko Cape Verde, huku wachezaji wengine wa kimataifa
wakitarajiwa kuwasili nchini kujiunga na timu muda wowote kuanzia leo.
''Tunatarajia
wachezaji wetu wanaocheza soka nje ya nchi watajiunga na timu muda
wowote kuanzia leo lakini nahodha wetu Mbwana Samatta ataungana na timu
huko Cape Verde'', amesema Ndimbo.
Mbali
na hilo Ndimbo amemshukuru kocha wa Lipuli FC Selemani Matola kwa
kuwaruhusu moja kwa moja wachezaji wake wawili Ally Sonso na Paul
Ngalema kujiunga na kambi bila kutoka kwenda kuichezea timu hiyo ambayo
leo inakipiga na Stand United.
Mbwana
Samatta jana alikuwa uwanjani kuichezea klabu yake ya KRC Genk kwenye
mchezo wa Europa League kundi I, ambapo ilikubali kichapo cha mabao 3-1
ugenini dhidi ya Sarpsborg 08 ya Norway.
Taifa
Stars inatarajia kucheza mchezo wake wa tatu katika kundi L kuwania
ufuzu AFCON 2019 dhidi ya Cape Verde mjini Praia, 12 Oktoba kabla ya
mchezo wa marudio utakaopigwa Jumanne 16, Oktoba jijini Dar es Salaam.
Tanzania inashika nafasi ya 2 ikiwa na alama 2 nyuma ya Uganda yenye
alama 4.
Comments