Millya alijiuzulu nafasi hiyo na uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani huku akitangaza kurejea CCM.
Millya ambaye alimshinda Christopher Ole Sendeka (CCM) katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 ametangaza uamuzi huo jana Oktoba 7, 2018 katika barua yake kwenda kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Katika barua hiyo, Millya alisema amekuwa mwanachama wa Chadema kwa miaka sita baada ya kuhama CCM uamuzi aliouchukua kutokana na kiu ya kuitafuta haki wakati huo na jukwaa ambalo angeweza kupaza sauti kwa misingi ya hoja na kupambana na rushwa na ufisadi.
“Naandika barua hii nikiwa na uhalisia mwingine kabisa, kila mtu atakuwa shuhuda nimekuwa si mtu wa siasa za jukwaani kwa miaka hii mitatu,” alisema.
“Ni dhahiri kwamba nimepoteza imani na kukosa amani, mahali nilipo sipaoni tena kama ni jukwaa la kunituma na kuhamasisha kuwaletea maendeleo wana Simanjiro,” alisema Millya.
Alisema chama cha siasa kinapaswa kuwa taasisi yenye mwelekeo wa kiitikadi na inayowatuma wawakilishi akiwemo yeye kuwahamasisha wananchi kushirikiana na serikali kutafuta na kuleta maendeleo.
“Ukweli ambao nimeuishi umekuwa mchungu na kinyume na matarajio yangu. Najua siasa za siku hizi msingi wake si siasa safi na zinatufanya ukiwa mbunge wa upinzani kila jambo unapinga hata pale kazi nzuri imefanyika ni dhambi kuunga mkono na kutoa hamasa ya kuongeza juhudi,” alisema.
“Siasa hizi hazina afya kwa taifa letu na wananchi wa Simanjiro, licha ya changamoto za hapa na pale lakini ukweli usiopingika serikali ya CCM imefanya kazi kubwa chini ya Rais John Magufuli,” alisema.
Zanzibarleo.
Comments