Masauni kupeleka TAKUKURU polisi Tunguu.



WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema, itaiagiza Taasisis ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi juu ya changamoto iliyopo katika kituo cha polisi cha Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Yussuf Masauni wakati alipofanya ziara ya kukitembelea kituo hicho cha polisi cha Tunguu.
Alisema kuwa, uchunguzi huo anautoa kwa jeshi la polisi kwa sababu wameshindwa kujichunguza wenyewe kwa haraka na kuchelewa kuleta ripoti hiyo, hivyo TAKUKURU itafanya uchunguzi na kubaini kwanini jeshi la polisi limechelewa.
“Jeshi la polisi waliniambia kuwa wameshaanza kufanya uchunguzi na nilikuwa nikisuri ripoti kwa hamu kwa ajili ya kutoa maamuzi, lakini jambo linalonisikitisha ni kwamba utolewaji wa repoti hiyo unachelewa kwani ni muda mrefuumepita”, alisema.
Aidha Masauni alifahamisha kuwa, alipata fununu kuwa kuna watu wengine waliona kwamba wadharau agizo lake na badala yake waweze kujenga katika eneo hilo la kituo cha polisi lakini amehakikishiwa na polisi kuwa hakuna mtu anayeendelea na ujenzi.
“Kwa hali hiyo sasa mimi sijaridhika na hiyo kasi kwa sababu sijapewa taarifa yoyote juu ya hatua iliyofikiwa juu ya huo uchunguzi waliosema wenyewe wameshaanza kuufanya”, alieleza.
Alisema kuwa, suala hilo linampa mashaka juu ya dhamira ya dhati ya kufanya uchunguzi huo kwa haraka ambavyo yeye anataka na kwa jinsi ambavyo serikali ya awamu ya tano tunavyokwenda nayo.
Alifahamisha kuwa, tunatakiwa kulinda rasilimali za wananchi na mwisho wa siku eneo hilo ni la wananchi ambao wanalipa kodi ambazo zinatumika kuwalipa mishahara jeshi la polisi.
Zanzibarleo.

Comments