Mapato yapaa TRA Zanzibar.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kanda ya Zanzibar imekusanya shilingi bilioni 68.3 sawa na asilimia 97 kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu.
Aidha kwa mwaka 2018-2019 Mamlaka hiyo inatarajia kukusanya shilingi bilioni 301.5.
Ofisa elimu na huduma kwa wateja, Abdalla Seif Abdalla, aliyasema hayo ofisini kwake Mlandege wakati alipozungumza na Zanzibar Leo.
Alisema Mamlaka hiyo ilikuwa na malengo ya kukusanya shilingi bilioni 70.6 kwa kipindi hicho cha robo ya kwanza.
Alisema fedha hizo zinatokana na kodi mbalimbali ikiwemo ulipaji kodi kwa wafanyabiashara.
Aidha alisema wameweka mikakati ya kusajili wafanyabiashara wapya na kuendelea na hatua ya kuwatembelea wateja wa zamani ili kufanikisha kuvuka malengo ya ukusanyaji kwa mwaka huo wa fedha.
Alifahamisha kuwa fedha hizo zimeingia kwenye mfuko mkuu wa hazina wa serikali.
Alisema fedha hizo zitaisaidia serikali kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa wakati ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, huduma za maji safi na salama, ujenzi wa skuli, huduma ya umeme na huduma nyengine za jamii.
Sambamba na hayo aliwataka wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha serikali kutimiza majukumu yake iliyojipangia kwani ulipaji wa kodi ndio unaowezesha kufikia maendeleo na ukuaji wa uchumi katika nchi.
Wakati huo huo wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja, wamepongeza utendaji kazi kwa watendaji wa ofisi hiyo kwa kuweza kukusanya kiasi hicho cha fedha ambapo walisema fedha hizo zitasaidia kutatua changamoto za wananchi kupitia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Zanzibaleo.

Comments