Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally amesema kwa mara ya
kwanza katika historia ya Tanzania, mwaka 2010 nchi ilipata Serikali
ambayo haikuwa na uhalali wa kisiasa.
Dk.
Bashiru aliyasema hayo jana mjini Morogoro, alipokuwa akitoa mada
katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata)
lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro.
Alisema
Serikali hiyo ilipatikana kwa sababu zaidi ya asilimia 50 ya wapigakura
waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza siku ya uchaguzi.
Katika
uchaguzi wa mwaka 2010 ambao Jakaya Kikwete alichanguliwa kuongoza
Serikali kwa awamu ya pili, wapigakura waliojiandikisha walikuwa
20,137,303 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa 8,626,283 sawa na
asilimia 42.84.
Jana
akizungumza mjini hapa, Dk. Bashiru alisema; “jambo la nne ninalotaka
kuzungumza ni uwajibikaji, mna nafasi gani ya kusimamia Serikali ili iwe
upande wenu, kwa sababu ukweli ni kwamba mamlaka ya Serikali yako
mikononi mwa umma na umma ni walio wengi ambao ni ninyi.
“Na
vyeo vyote vilivyopo Serikali ni mali yenu, isipokuwa kuna mchakato wa
usimamizi wa vyeo vyenu kupitia Serikali na moja ya michakato ni
uchaguzi, hebu tujiulize tabia yenu na mwenendo wenu wakati wa uchaguzi
ikoje?
“Tuambizane
ukweli, mkishapewa kofia na T-shirt (fulana), alafu nyimbo zikaanza
kupigwa za ‘mbele kwa mbele’, huwa mnapata nafasi za kuhoji sifa za
mnayetaka kumchagua?
“Je, sifa ya chama mnachotaka kukichagua kinachopiga ‘mbele kwa mbele’ unaijua?
“Kwa
hiyo eneo jingine muhimu kwa nafasi yenu ni kuwa sehemu ya mchakato ya
kuwajibisha wote wenye vyeo vyenu. Kwahiyo msichague kiongozi kwa
T-shirt, kwa kofia, kwa ubwabwa, kwa pesa.
“Kwa
kufanya hivyo mnatengeneza watu watakaokuja kuwaonea, kwa sababu
dhuluma zote na uonevu hazifanywi na wakoloni, zinafanywa na wale
mliowachagua nyie wenyewe. Au wale walioteuliwa na wale mliowachagua.
“Sasa
watu ambao ni wajanja, mimi naweza kusema wapigakura wa Tanzania ambao
wamefikia hatua ya kudharau uchaguzi, wanakaa nyumbani (siku ya
uchaguzi) kwa sababu wanaona ni kama kituko, ni mchezo wa kuigiza.
“Na
ndiyo maana leo kupata watu kuhudhuria kupiga kura imekuwa shida, kote
tunakoshinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40, hakuna
mahala ambako wapigakura wamejitokeza kwa zaidi ya asilimia 50.
“Na
mwaka 2010 ilitia fora, watu wengi walijiandikisha zaidi ya asilimia
100, kumbe walikuwa wanataka kile kipatarata (kitambulisho cha
mpigakura) kwa sababu kinatumika kwenda polisi kudhamini,
unajitambulisha, walipokipata wakaingia mitini.
“Kwa
mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, tulipata Serikali ambayo
haikuwa na uhalali wa kiasiasa kwa sababu wapiga kura wengi zaidi ya
asilimia 50 walibaki nyumbani na tatizo hili halijaisha, lakini
mwanasiasa akishashinda anasema ushindi ni ushindi tu hata kama ni kwa
kura moja.
“Hajali
kwamba ushindi ule unatakiwa uwe na uhalali, tulifika mahala ambapo
ikifika wakati wa uchaguzi wagombea wanauza nyumba, wanakopa, wanaitisha
mikutano ya kuchangisha, usipomchangia mkali utafikiri anakwenda
hospitali kutibiwa.
“Akishazikusanya
zile fedha anaenda kuwanunua mawakala na mawakala wanawanunua
wapigakura, msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi,
ninachowaomba nafasi yenu ni kubomoa na kuharibu soko la kura.”
Dk.
Bashiru alisema kwa sababu kama CCM itakuwa imejipanga, mipango mizuri
ya kuhudumia umma ipo, wananchi wanaona shule, hospitali hakuna haja ya
kwenda kuhonga.
“Ukiona
mtu anakuhonga hana sifa, na ndani ya CCM tumeshasema itakuwa sababu ya
kutoteua mtu huyo hata kama atakuwa ameshinda kura za maoni.
“Kwa
sababu bila kuwa na mfumo wa kuwapata viongozi, na nasikia sasa hivi
rushwa imeenda mpaka kwa wenyeviti wa vijiji, kitu ambacho ni hatari,
kwa sababu mwenyekiti wa kijiji anasimamia mazingira na wananchi wake,
anasimamia migogoro na wananchi wake, anasimamia haki na wananchi wake,
akianza kununua uongozi atauza ardhi.
“Kwahiyo
mambo haya manne kwangu mimi naona ni muhimu sana, ili uweze kupata
nafasi katika uchumi wa taifa hili, uwezo wenu wa kutambua mambo,
kutambua kwamba benki ya ardhi ni wizi, kwamba bodi za mazao ni wizi na
mimi nashangaa mpaka leo Bodi ya Kahawa ipo,” alisema.
Mpekuzi.
Comments