Kamanda Mambosasa Atoa Onyo kwa Bodaboda Dar....60 Watiwa Mbaroni Kwa Kuhujumu Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco).

Jeshi  la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limeanza operesheni maalumu ya kukamata bodaboda zote zinazoingia katikati ya Jiji ambapo ndani ya saa 24 wamekamata pikipiki 104.

Hayo yamesemwa jana  na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa wakati anazungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni ambazo wanazifanya.

Alisema  Polisi wameanza operesheni ya kukamata waendesha bodaboda ambao wanaingia katikati ya mji wakati wamezuiliwa kuingia mjini.

Kamanda Mambosasa alisema baadhi ya bodaboda ambazo zimekamatwa zimetokana na makosa ya kutovaa kofia ngumu kwa wanaoendesha,kupitia njia tofauti na utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na kupakia mishikaki.

"Ni marufuku bodaboda kuingia katikati ya Mji,hatuwezi kuacha hilo likaendelea kufanyika.Walishakatazwa kuingia katikati ya mji." Alisema Mambosasa na kuongeza;

"Mbali ya kuwakamata wanaiongia mjini pia tunaendelea na operesheni ya kukamata bodaboda ambazo zinatumika kutenda matukio ya uhalifu.Pia tutakamata bodaboda ambazo wanaoziendesha wanashindwa kufuata sheria za usalama barabarani."

Wakati huo huo Mambosasa amesema Polisi kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco) wamefanikiwa kukamata watu 60 ambao wanatuhumiwa kujihusisha na kuhujumu miundombinu ya umeme na kujiunganishia umeme bila utaratibu na kuchezea mita za Luku.

Kamanda Mambosasa alisema wapo ambao wamefikishwa mahakamani na wengine wanaendelea kuhojiwa na kisha watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Alisema kuwa wanaojihusisha na kuhujumu miundombinu ya umeme wafahamu opereshenii hiyo ni endelevu na kwamba watakaoendelea wajue wao ni wafungwa watarajiwa kwani hawatabaki salama.
 
Mpekuzi.

Comments