Dk. Shein: Maonesho ya utalii kuitangaza Z’bar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema maonesho ya utalii yanayofanyika Zanzibar ni muhimu kwani yamelenga kuitangaza Zanzibar kiutalii ambao ndio muhimili wa uchumi.
Aliyasema hayo jana katika viwanja vya hoteli ya Verde, Mtoni katika ufunguzi wa maonesho ya utalii Zanzibar ya mwaka 2018 ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wadau wa utalii.
Alisema utalii unachangia asilimia 27 ya pato la taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazokusanywa ambapo muda wanaokaa watalii nchini umeongezeka ambapo mtalii hutumia wastani wa siku 8 badala ya 6 kama ilivyokuwa miaka 5 iliyopita.
Alifahamisha kwamba takwimu hizo ni njema na zinaonesha jinsi sekta ya utalii inavyokua kwa kasi kwa watalii kupenda kubakia nchini huku wakiwa tayari kutumia fedha wanazokuja nazo.
Alieleza juhudi mbali mbali za kuimarisha utalii zinazoendelea kuchukuliwa na serikali zikiwemo kuanzisha mpango wa “utalii kwa wote” ambapo lengo lake ni kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inawanufaisha wananchi wa Zanzibar na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Alisisitiza kuwa juhudi mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa na serikali za kuendeleza sekta ya utalii ambazo zinakwenda sambamba na mikakati na malengo ya MKUZA, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 na malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Alieleza imani yake kwamba maonesho hayo ni njia bora ya kuitangaza Zanzibar na fursa mbalimbali zilizopo za kiuchumi kwa wawekezaji ambapo pia, washiriki watazifahamu fursa hizo.
Alisema Zanzibar imejaaliwa na mazingira yanayovutia na ina vivutio vingi vya utalii zikiwemo fukwe na sehemu za historia pamoja na hoteli nyingi za kisasa ikiwemo hoteli hiyo ya Verde.
Alitumia fursa hiyo kueleza juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kuzijenga upya na kuzifikisha katika maeneo muhimu ya utalii kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo sambamba na shughuli za uwekezaji na huduma kwa wananchi.
Zanzibarleo.

Comments