Dk. Shein afunga kampeni Jango'mbe.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema, serikali aliyokabidhiwa kuiongoza na wananchi kupitia ilani ya CCM, imeweza kutekeleza kwa vitendo masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kijamii yenye maslahi ya wananchi wote.
Alisema kuna utekelezwaji mzuri wa ilani ya CCM ambao umefanikisha kupatikana maendeleo katika majimbo yote Unguja na Pemba, pamoja na kuwepo baadhi ya chagamoto ambazo zinatatuliwa awamu kwa awamu.
Dk. Shein aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza na wana-CCM na wananchi wa jimbo la Jang’ombe kwenye hafla ya ufungaji wa kampeni ya uwakilishi wa jimbo hilo, kupitia CCM katika kiwanja cha Matarumbeta.
Alisema sehemu za jimbo hizo zimekuwa zinabadilika kwa wakati, ambapo maendeleo yamekuwa yakipatikana na watu wamekuwa wanayaona kwa vitendo.
Aliwaahidi wananchi wa Jang’ombe kuwa serikali itaitengeneza skuli ya Kidongo Chekundu, kwani fedha za kutosha za ujenzi wa skuli hiyo zipo hali ambayo itawawezesha watoto wa eneo hilo waweze kuitumia kwa kujipatia elimu ambayo itaongoza maisha yao.
Aidha alisema changamoto za maji hazipo katika jimbo la Jang’ombe tu, bali maeneo mengi na kwamba serikali itaendelea na mipango yake ya kuzitatua ili wananchi waweze kuondokana na shida hiyo.
Zanzibarleo.

Comments