Mkataba wa CRDB na mtaalamu huyo wa uchumi na masuala ya fedha unatarajiwa kukamilika Mei 31 mwakani na kwa muda huu wote alikuwa anatakiwa aendelee na majukumu yake.
“Amechukua garden leave (likizo ya kuacha kazi),” alisema Tully Mwambapa ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko na Huduma wa CRDB alipoulizwa na Mwananchi kuhusu habari zilizoenea jana asubuhi kuwa Dk Kimei amejiuzulu.
Garden Leave ni likizo ambayo hutumiwa na waajiri, hasa benki au taasisi za kifedha kumuelekeza mfanyakazi anayeondoka kazini au aliyeachishwa kazi, kuwa mbali na kazi hadi muda wake utakapofika, huku akiendelea kupata haki zake.
Utaratibu huu hutumika kumzuia mfanyakazi anayeondoka kazini kujua taarifa hasa muhimu za maendeleo ya taasisi wakati akiondoka kwa muajiri wake na hivyo kuzuia uwezekano wa kutumiwa na wapinzani wa muajiri wake wa sasa iwapo atajiunga nao.
Kimei amechukua likizo hiyo miezi mitatu kabla ya kuanza kukabidhi majukumu kwa mrithi wake.
Desemba mwaka jana, Dk Kimei alitangaza nia yake ya kustaafu na kuipa benki hiyo miezi 19 kumtafuta mrithi wake. Muda huo ulikuwa na ziada ya mwezi mmoja kulingana na utaratibu wa CRDB ambao ni miezi 18.
Hata hivyo, siku tatu baada ya kutambulishwa na kupokewa kwa Abdulmajid Nsekela ambaye amekuwa bosi mpya wa CRDB, Dk Kimei amejiondoa katika majukumu ya kila siku ya benki hiyo baada ya kuiongoza kwa zaidi ya miongo miwili na kuipa mafanikio makubwa kwenye sekta ya fedha na uchumi.
Mwezi uliopita, bodi ya wakurugenzi wa CRDB ilimtangaza Nsekela kuwa mkurugenzi mtendaji mpya wa benki hiyo.
Taarifa ya mwenyekiti wa bodi hiyo, Ally Laay ilisema Nsekela ataanza kukabidhiwa ofisi mapema mwakani na kazi hiyo itakamilika Mei wakati Dk Kimei atakapostaafu. Kinyume na matarajio hayo, mchumi huyo mwandamizi ameamua kujiweka kando.
Hata hivyo, Tully alisema kwa miezi iliyobaki, Dk Kimei ataendelea kumpa Nsekela ushirikiano unaohitajika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake.
“Atakuwa anamsaidia kutoka nyumbani,” alisema.
“Itakumbukwa kuwa Dk Kimei amemlea kitaaluma Nsekela miaka ya nyuma alipokuwa anafanya kazi na benki hii. Ataendelea kumsaidia kila atakapohitaji.”
Nsekela ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 na wakati anateuliwa kuiongoza CRDB ambayo ukubwa kwa amana zake ni zaidi ya Sh5 trilioni, alikuwa mkurugenzi wa wateja wadogo wa benki ya NMB.
Uzoefu wa miaka 10 kati ya hiyo aliupata akiwa CRDB alikoanzia kazi mwaka 2007 kabla ya kujiunga na NMB.
Mapema Machi, alipokuwa anafungua tawi jipya la CRDB Chato, Rais John Magufuli aliahidi kumpa Dk Kimei majukumu.
“Nasikia unastaafu huko CRDB. Tunakusubiri kwani Serikali bado inakuhitaji,” alisema.
Comments