CCM Jang’ombe yashinda kwa 90.5%.

MGOMBEA wa kiti cha Uwakishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Jong’ombe, Ramadhan Hamza Chande ameshinda nafasi hiyo kwa kupata jumla ya kura 6,581 ambazo ni sawa na asilimia 90.5.

Akitangaza matokeo hayo, matokeo ya uchaguzi huo, jana jioni Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Jang’ombe Mwanapili Khamis Mohamed alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi anamtangaza mgombe huyo kuwa mshindi kwenye uchaguzi huo.

Alisema kuwa Ramadhan Hamza Chande kutoka CCM, amepata kura 6,581 katika jumla ya kura 7,274 zilizopigwa kwenye uchaguzi huo uliofanyika hapo jana.

Mwanapili aliongeza kuwa matokeo kura kwenye (mabano) ya vyama vyengine Chama cha AAFP (58), ADA TADEA (131), CCK (73), CUF (172), DP (73).

Hapo jana wananchi wa jimbo la Jang’ombe wamejitokeza kwa wingi katika zoezi la uchaguzi mdogo la kumchagua mjumbe wa Baraza la Wawakilishi atakayeliongoza jimbo hilo kufuatia aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, Maulid Abdalla Diwani kuvuliwa uanachama na Chama cha Mapinduzi.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi hao waliofika vituoni kupigia kura walisema wameridhishwa na hali ya ulinzi na usalama, hali ambayo imewapa fursa kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Simai Mohamed Simai alisema katika kituo chake kulikuwa hakuna usumbufu wa aina yoyote ambapo alikwenda na kupewa karatasi ya kura na kumchagua kiongozi anayemuona anafaa.

Kwa upande wake, msimamizi wa uchaguzi jimbo la Jang’ombe, Mwanapili Khamis Mohamed, alisema zoezi la upigaji kura limeanza vyema kama utaratibu uliopangwa na Tume ya Uchaguzi ya Uchaguzi.

Alisema kuwa katika vituo hivyo hakuwa na malalamiko yaliyojitokeza katika zoezi zima la uendeshaji wa uchaguzi ambapo hali imekwenda kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili kutumia fursa ya kumchagua kiongozi wanayemtaka aweze kuwatumikia katika jimbo hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Taifa, Athumani Kihamia, alisema amesema kuwa Tume yao ilijiridhisha kuwa vituo vimefunguliwa kwa utaratibu uliowekwa saa 1:00 asubuhi na alishuhudia kuwa wapiga kura walijitokeza mapema kwenda kutekeleza haki yao ya msingi.

Comments