Balozi Seif: Nidhamu michezoni msingi wa mafanikio.

MAKAMU wa  Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Sef Ali Iddi,  amewahimiza wanamichezo kuendeleza nidhamu katika michezo kwa vile inaendeshwa kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizoridhiwa na vyama ulimwenguni.
Hayo aliyaeleza alipokuwa akizungumza na wanamichezo katika uwanja wa Amaan baada mchezo wa fainali ya Bonanza la Ujamaa ambapo Ujamaa iliibuka na mabingwa kwa kuifunga Mlandege bao 1-0.
Alisema ni vyema kwa wanamichezo kufuata sheria na taratibu za michezo zinazosimamiwa na mwamuzi ambaye yeye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho,hivyo,  hawanabudi kutunza nidhamu kwa anayoyamua wakati anapokuwa uwanjani.
“Maamuzi ya  mwamuzi ni  ya mwisho, mkubaliane nayo na huo ndiyo uanamichezo”, alisema.
Balozi Seif, alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwatunza vijana na wanamichezo kwa lengo la kufikia malengo wanayoyatarajia kucheza kitaifa na kimatafa.
Aidha, Balozi Seif, alieleza kuvutiwa na kiwango cha soka kilichoshuhudiwa kwenye mashindano hayo na hivyo kutoa taswira bora ya soka la Zanzibar.
“Ushahidi wa hilo ni jinsi Zanzibar Heroes ilivyoibuka mshindi wa pili kwenye Kombe la Chalenji” alisema.
Pia aliishukuru na kuipongeza timu ya soka ya Ujamaa kwa umahiri wake wa kuandaa bonanza hilo lililozishirikisha timu kadhaa hapa nchini.
Aidha, Balozi Seif aliwapongeza Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kwa kuwaandaa vijana wa akademia kwa umakini na kuwa na uwezo wa kuchezesha mpira wakiwa na ufanisi mkubwa.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa wilaya ya Mjini, Marina Thomas kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, alisema, Ujamaa ni timu yenye historia kubwa kutokana na kuwashirikisha watu mashuhuri visiwani.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema,  ushindi wa vijana wa Ujamaa umethibitisha wazi kwa kuitendea haki klabu hiyo kutokana na shindi huo ambao utawajengea mwanzo mzuri wa kurejea kwenye hadhi yao  iliyokuwepo miaka ya nyuma.
Zanzibarleo.

Comments