Katika kipindi hiki, wataalamu wa ugonjwa huo kutoka Wizara ya Afya na Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar, watakuwa na kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuufahamu na jinsi ya kujikinga. Kilele kitafanyika Oktoba nne katika kijiji cha Jambiani ambapo shughuli ya kuwachanja mbwa, itafanyika.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Amina Makame Haji, Ofisa Afya kutoka Idara ya Kinga katika Wizara ya Afya, alisema kichaa cha mbwa (rabies) ni ugonjwa unaosababishwa na virusi (lyssavirus) ambao wana uwezo wa kuathiri wanyama wanaofugwa na kuusambaza kutoka kwa mnyama alieambukizwa kwenda kwa binaadamu.
Alisema virusi hao huambukiza kwa kupitia mate, ambapo mnyama alieathirika atakapotafuna au kuramba mnyama mwengine au binaadamu, virusi hao huhama kutoka kwa mnyama alieathirika kwenda kwa mnyama mwengine au binaadamu.
“Ugonjwa wa kichaa cha mbwa hutoka kwa mbwa kwenda kwa wanyama wengine wanaofugwa kama ng’ombe, mbuzi na binaadamu, hawa wote wana uwezo wa kupata ugonjwa huu pindipo watatafunwa au kurambwa na mbwa alieambukizwa,” alisema.
Alisema kirusi huyo anapoingia kwenye mwili wa binaadamu au mnyama, anaathiri ubongo na hapo ndipo dalili za ugonjwa huo huanza kuonekana.
Alisema dalili za ugonjwa huo huonekana baada ya siku 10 hadi 20 hadi mwezi mmoja tokea mtu au mnyama alipotafunwa au kurambwa na mbwa inategemea na ukubwa wa jeraha.
Alisema mtu alietafunwa kichwani, dalili za ugonjwa huo huonekana haraka tofauti na mtu alietafunwa mguuni au sehemu nyengine za mwili.
Alisema dalili za ugonjwa huo ni homa kali, maumivu makali ya kichwa, kutoka mate na wakati mwengine aliembukizwa huogopa hata kuangalia maji.
Nae Dk. Khadija Noor Omar,kutoka Idara ya Maendeleo ya Mifugo, alisema chanzo cha ugonjwa huo ni mbwa lakini mnyama yoyote mwenye damu moto, anaweza kuambukizwa.
Zanzibarleo.
Comments