Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango ameuagiza uongozi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, kuwachukulia hatua kali za kisheria na
kinidhamu wafanyakazi wake wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa
maadili ikiwemo rushwa na kutumia njia zisizokubalika wakati wa
kukusanya kodi za Serikali.
Dkt.
Mpango ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TRA
Mkoa wa Tanga, ambapo ameagiza wafanyakazi wawili wa mamlaka hiyo,
Robinson Munisi na Abraham Maleko waondolewe kwenye kazi wanazofanya
sasa na kupangiwa kazi nyingine baada ya kuwepo kwa tuhuma za ulevi wa
kupindukia na kujihusisha na mtandao wa wafanyabiashara unaotumika
kuikosesha Serikali mapato yake
Amewataka
watumishi wa mamlaka hiyo kuwa waadilifu kwa kujiepusha na vitendo vya
rushwa na lugha za kuudhi kwa wateja wao ili kupunguza malalamiko kutoka
kwa walipa kodi na kuonya kuwa serikali haitomvumilia mtumishi yeyote
atakayefanya kazi kinyume na maadili ili kujenga nidhamu kwa watumishi
hao na hatimaye kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato ya Serikali.
“Mwambieni
Kamishna Mkuu wa TRA (Bw. Charles Kichere) kwa watumishi hawa siwataki,
wapelekeni maeneo mengine mbali huko na muendelee kuwachunguza, na
nataka kupata taarifa ya watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya
utumishi wa umma ikiwemo kujihusisha na rushwa” alisisitiza Dkt. Mpango
Aidha,
amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na
Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles Kichere, kuhakikisha boti la doria
katika Mwambao wa Bahari mkoani Tanga linapatikana haraka ili kuzuia
biashara ya magendo inayoyofanywa kwa kutumia bandari bubu hivyo
kuikosesha Serikali mapato yake.
“Ni
lazima jambo hili lifanyike haraka kwa sababu ya umuhimu wake kwasababu
si tu kwamba Serikali inapoteza mapato yake kutokana na vitendo hivyo
vya kuvusha magendo kupitia bandari bubu lakini pia ni hatari kwa
usalama wa Taifa kwa sababu maadui wanaweza kupitisha silaha” alionya
Dkt. Mpango.
Akisoma
taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Mamalaka hiyo, Meneja wa TRA
Mkoa wa Tanga Bw. Masawa Masawa alisema makusanyo ya Mkoa huo yamekuwa
yakiongezeka Mwaka hadi Mwaka kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka
2013 hadi 2017 ambapo katika Mwaka 2016/17 Mkoa ulikusanya Shilingi
bilioni 107.39 kati ya Shilingi bilioni 131.06 ya malengo kwa Mwaka huo
ambayo ni sawa asilimia 82 ya makusanyo.
Kuhusu
maadili ya wafanyakazi wa Mamlaka hiyo mkoani Tanga, Bw. Masawa amesema
kuwa pamoja na kuwapa elimu kuhusu maadili mema kupitia Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU, wamekuwa wakiwachukulia hatua
kali watumishi wao wanaobainika kujihusisha na vitendo vinavyochafua
taswira ya mamlaka hiyo.
Akihitimisha
mkutano huo, Dkt. Mpango, alimwagiza Meneja huyo kupandisha kiwango cha
ukusanyaji mapato kwa asilimia 100 na kutoa onyo kwa Mameneja wote wa
TRA nchini watakaoshindwa kufikia lengo hilo wajitathmini kama wanatosha
kwenye nafasi zao.
Mpekuzi.
Comments