WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanajiosayansi nchini wawe walinzi wa
kwanza wa rasilmali za madini, maji na mafuta bila kujali wako
serikalini au kwenye sekta binafsi.
“Katika
utendaji wenu wa kazi, mnapaswa kuwa wa kwanza kujua kinachoendelea
katika sekta zote mnazohusiana nazo, yaani madini, maji na mafuta.
Haijalishi unafanya kazi serikalini au shirika binafsi, wewe ni
Mtanzania na una jukumu la kulinda rasilimali za nchi yako.” amesema.
Waziri
Mkuu ametoa wito huo jana mchana (Alhamisi, Septemba 27, 2018), wakati
akifungua warsha ya siku sita yaJumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania
iliyoanza leo kwenye hoteli ya New Dodoma, jijini Dodoma.
Waziri
Mkuu ambaye amefungua warsha hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, amewataka wanajiosayansi hao kutoka Serikalini, taasisi
binafsi na vyuo vya elimu ya juu wasishiriki kulihujumu Taifa kwani kwa
kufanya hivyo, watakuwa wasaliti namba moja.
“Msijihusishe
au kushiriki kulihujumu Taifa lenu kwani kwa kufanya hivyo, mtakuwa
wasaliti namba moja. Hakikisheni mnakuwa mabalozi wa Serikali katika
mashirika haya kwa kutoa elimu juu ya sheria zinazosimamia sekta hizi
huku mkisisitiza umuhimu wa kufuata sheria za nchi zenye kusimamia
rasilimali zetu adhimu,” amesema.
Amesema
mbali ya kilimo, rasilmali miamba na madini ndivyo vyenye mchango
mkubwa wa kukuza viwanda kote duniani na kwamba utaalamu wa jiosayansi
una mchango mkubwa kwenye malighafi za viwandani, upatikanaji wa maji ya
kutosha nchini, mafuta, gesi asilia na uzalishaji wa nishati kupitia
jotoardhi.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wanajiosayansi hao waisaidie
Serikali kutafuta vyanzo vya maji vya uhakika ili itumie kihalali fedha
zinazotengwa kwenye uchimbaji visima vya maji na kuepuka upotevu wa
fedha.
“Ni
jukumu la wanajiolojia la kutuambia wapi maji yapatikana. Muandae
utaratibu mzuri wa kutunza takwimu kuhusu kiwango cha maji, ni wapi maji
yalipo na ujazo wake. Kwenye eneo hili tumepoteza fedha nyingi sana,
tumepeleka fedha nyingi kwenye halmashauri ili tutoe huduma za maji
wananchi lakini kwa sababu hatukuwashirikisha wanajiosayansi, wachimbaji
wameenda kuchimba visima na wakakosa maji, yakabaki mashimo tu bila
maji. Mna jukumu kubwa la kuisadia Serikali ili itumie vizuri fedha
inazozitenga kwa ajili ya maji kwa kubainisha wapi kuna maji, yako kiasi
gani na yako umbali gani,” amesema.
Wakati
huohuo, Waziri wa Madini, Bibi Angella Kairuki amesema wizara hiyo
inakusudia kuanzisha chombo maalum cha usajili cha kuwatambua
wanajiosayansi kisheria kupitia Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi nchini
(Geoscientists Registration Board -GRB) kama ilivyo kwa wahasibu,
wahandisi na mabaraza ya wasajili mbalimbali ili kukabiliana na
wataalamu feki wa fani hiyo.
“Wizara
ya Madini inategemea wanajiosayansi wawe wazalendo kwa Taifa kwa kutoa
taarifa za kitaalamu zinazoendama na uhalisia ili kuondoa malalamiko
yanayotokana na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu hasa wale
wanaojifanya wataalamu ilhali wakijua wazi hawana utaalamu wa fani hii,”
amesema.
Amesema
azma ya Serikali ni kumaliza changamoto zinazoikabili sekta hiyo ya
madini zikiwemo ukiritimba uliokuwa ukifanyika katika mlolongo mzima wa
utoaji leseni, utafutaji na uzalishaji wa rasilmali madini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Mpekuzi.
Comments