
Ulaya,Urusi na China zimejiweka katika nafasi ya kuvutana na rais wa
Marekani Donald Trump baada ya hapo jana usiku kutangaza mipango ya
kuunda njia maalum za kurahisisha shughuli za kibiashara na Iran,hatua
ambayo inakiuka vikwazo vya Marekani.
Baada ya mkuu wa sera za
nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kukutana na wajumbe kutoka
Uingereza,Ufanasa,Ujerumani ,Urusi China na Iran hapo jana alitangaza
kwamba nchi hizo ambazo zote zimesaini makubaliano ya Nuklia ya Iran
zimefikia uamuzi wa kuendelea na shughuli za kibiashara na
Iran.Akafafanua zaidi kwa kusema:
''Washiriki
wamesisitiza haja ya kulinda uhuru wa uendeshaji wa kiuchumi ili kuwa na
fursa ya kufanya biashara kwa njia halali na Iran kwa kuzingatia kwa
ukamilifu azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa nambari 2231''
Maamuzi
yaliyofikiwa na nchi hiyo yanamaanisha kwamba sasa Umoja wa Ulaya
utaunda taasisi huru ya kisehria ambayo itaratibu shughuli kutowa na
kupokea malipo ya fedha katika shughuli za kibiashara na Iran.
Mogherini
aliendelea kusema kwamba kundi hilo la nchi Umoja wa Ulaya,China na
Urusi zimeidhinisha kwa kauli moja mapendekezo ya kiutendaji ya
kuendelea kuzibakisha na kuziimarisha njia za kurahisisha mchakato wa
malipo yanayohusiana na biashara na Iran ikiwemo biashara ya mafuta.
Nchi
zote zilizoshiriki katika mkutano uliofikia maamuzi hayo jana ziliafiki
kwamba Iran inatekeleza majukumu yake kama sehemu ya mkataba wa Nyuklia
uliosainiwa 2015 na hilo limethibitishwa katika ripoti 12 mfululizo
zilizowahi kutolewa na shirika la kimataifa la Atomiki IAEA.
Lakini
hatua iliyochukuliwa na nchi hizo ni dhahiri inaweka mazingira ya
kuzuka mvutano mkubwa na Marekani ambayo iliiwekea tena vikwazo Iran
mnamo mwezi Agosti ambavyo pia vinataja kwamba nchi yoyote au makampuni
yatakayoshirikiana kibiashara na Iran yataadhibiwa.
Duru nyingine ya
vikwazo vya Marekani kuelekea Iran inatarajiwa kutangazwa mwezi Novemba
na hasa vikilenga kukwamisha kabisa usafirishaji wa mafuta wa jamhuri
hiyo ya kiislamu.
Vikwazo hivyo vitamaanisha kwamba makampuni
zaidi makubwa yatalazimika kuamua ama kuondowa vitega uchumi vyao Iran
au kupoteza fursa zao za kibiashara na Marekani.
Jana waziri wa mambo ya
nje wa Marekani Mike Pompeo alifanya mkutano na waandishi habari
akasema kwamba rais Trump atatumia nafasi yake kama mwenyekiti wa baraza
la usalama la Umoja wa Mataifa kuzitolea mwito nchi zote kuunga mkono
kampeini ya kuishinikiza Iran katika mpango wake wa Nyuklia.
Uamuzi huo
wa Marekani lakini huenda ukasabababisha cheche za moto na wanachama
wengine wa baraza la usalama la Umoja huo wa Mataifa,Uingereza,Ufaransa
China na Urusi.
Comments