Kwa mujibu wa takwimu za kipindi cha mwaka mmoja wa mradi wa THP’s unaosimamiwa na kutekelezwa na taasisi za Zanzibar Youth Forum (ZYF) na ZAYEDESA kutoka 2017 hadi 2018 maambukizi ya VVU kwa mkoa wa Mjini Magharibi yameongezeka.
Akizingumza kwenye mkutano wa wadau wa makundi maalum (KPs) katika ukumbi wa THP’s jengo la Muzamili Mlandege mjini Unguja, Meneja Miradi ZAYEDESA, Mgoli Mgoli wakati akiwasilisha kwa wadau hao, changamoto na mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi chote cha mradi huo, alisema kutoka Oktoba hadi Disemba 2017, THP’s uliwafikia watu 1,342 na kuwapima 1,291 hati yao 104 waligundulika na VVU ambapo 89 kati yao walifikishwa kwenye vituo vya kuwapatia huduma na 10 walikimbia.
Alisema hadi mwaka 2012 maambukizi ya UKIMWI kwa Zanzibar yalikuwa ni asilimia moja kwa wakazi wake 1.3 milioni.
Akitoa ufafanuzi wa maambukizi ya VVU, Mgoli alieleza kuwa kwenye makundi maalum (KPs) kwa ujumla kuna maambukizi ya asilimia 33. 4 ambapo kaka poa wameathirika kwa asilimia 2.6, dada poa asilimia 19.3, wateja wanaojidunga sindano asilimia 11.5.
Alisema mradi wa THP’s ulijikita kwa Mkoa wa Mjini Magharibi kutokana na kuwemo kwa asilimia 50 ya makundi hayo pamoja na muingiliano wa watu.
Alieleza kuna mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi chote cha mradi huo ikiwemo kutoa huduma bure za kupima HIV baada ya kuifikia jamii kubwa zaidi.
“Tulipozigundua kesi za walioathirika tuliwachukua mguu kwa mguu na kuwafikisha kwenye huduma kwa lengo la kuwasaidia watu kujisajili na kupata huduma kamilifu”, alieleza.
Aidha, mafanikio mengine ni kutoa elimu na hamasa kwa jamii ili kujenga uelewa juu ya athari za HIV sambamba na kufanikiwa kukusanya sindano nyingi chafu zilizokuwa zikitumiwa na makundi yanayojidunga kwa lengo la kuepusha maradhi ya homa ya ini ‘B’ na ‘C’ ambayo aliyataja kuwa ni hatari zaidi ya UKIMWI.
Zanzibarleo.
Comments