Ujenzi wa maabara, maktaba skuli 24 waanza.

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema wizara imeanza ujenzi wa vyumba vya maabara, maktaba na kompyuta kwa skuli 24 za Unguja na Pemba, kupitia mradi wa ZISP ukiwa na lengo la kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Chukwani.
Alisema kati ya skuli hizo, Unguja zipo 14 na Pemba 10 ambapo ni Mwanakwerekwe, Jang’ombe, Kisauni, Tunguu, Kijini, Mkwajuni, Donge, Mahonda, Kitope, Chuini, Bwejuu, Mtoni Kigomeni, Uroa na Unguja Ukuu.
Kwa upande wa Pemba ni Wingwi, Kiuyu, Makangale, Kisiwapanza, Mtambile, Kilindi, Pujini, Kojani, Fundo, na Limbani.
Alisema baada ya kumalizika kwa skuli hizo wataweka vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya matumizi.
Aidha alisema, wizara itakamilisha ujenzi wa skuli tisa za ghorofa zitakazokuwa na maabara za sayansi na kompyuta, ambapo tano zipo Unguja na nne Pemba.
Alisema wizara itahakikisha inasabaza vifaa vya maabara na vitabu kwa wakati na kuwataka walimu na wanafunzi kuvitumia ipasavyo ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi wao.
Alisema katika kuimarisha elimu nchini viongozi wa wizara hiyo walifanya ziara katika skuli za Unguja na Pemba ambapo skuli 162 zilikaguliwa.
Akitoa maoni ya Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shehe Hamad Mattar, aliitaka wiara kulifanyia kazisuala la stahiki za walimu ili kuondosha malalamiko.
Zanzibarleo.

Comments