‘Ujenzi soko la kuku Darajani kuongeza mapato’.

WAFANYABIASHARA wa kuku katika soko la Darajani, wametakiwa kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki cha ujenzi wa soko hilo na kutosikiliza maneno ya watu wengine wenye lengo la kuleta  mtafaruku kati yao na serikali.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Shamata Shaame Khamis, alisema hayo wakati akikagua soko hilo.
Alisema ujenzi wa soko hilo, unaendelea kama ulivyopangwa na sio kama wanavyodai baadhi ya watu kuwa ujenzi umesimama.
Alisema lengo kuu la serikali  kujenga soko hilo ni kuhakikisha soko hilo linaongeza mapato zaidi na wafanyabiashara wanafanya kazi katika mazingira.
Aidha aliliagiza baraza la manispaa ya mjini kuhakikisha wanawasimamia  vyema wauza vyakula (mama ntilie) ili wafanye kazi zao katika mazingira mazuri.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Maghraibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, aliwaomba viongozi kutoa taarifa   walizozifanyia uchunguzi ili kuondosha sintofahamu kwa wananchi.
Aliwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi juu ya ujenzi huo kwani serikali itahakikisha unakamilika kwa wakati.
Mkuu wa Idara ya Huduma za Jamii manispaa hiyo, Rajab Salum Rajab, alisema lengo la kujengwa soko hilo ni kuimarisha huduma za uchinjaji kuku.
Sambamba na hayo, alisema wafanyabiashara wa soko hilo na manispaa wanapata mapato kutokana na soko hilo, hivyo kuna kila sababu ya kuimarishwa.
 Zanzibarleo.

Comments