Tundu Lissu, Profesa Kabudi wavutana kuhusu uchunguzi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ameingia katika mvutano na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu juu ya tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa mwanasheria huyo wa Chadema mjini Dodoma.
Mvutano huo umeibuka baada ya Profesa Kabudi kusema uchunguzi wa tukio la Lissu unaendelea huku akitaja matukio ya aina hiyo yaliyowahi kutokea nchini Marekani ikiwamo mauaji ya aliyewahi kuwa Rais wa nchi hiyo, John Kennedy kwamba aliyehusika kumuua hajawahi kukamatwa.
Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi nje ya makazi yake jijini Dodoma, Septemba 7 mwaka jana akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge, anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji na uchunguzi wa tukio lake umekuwa ukielezwa na vyombo vya dola unaendelea kufanyika.
Septemba Mosi, Profesa Kabudi akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini Marekani, aliulizwa swali juu ya lilipofikia tukio la Lissu, ambaye amewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Profesa Kabudi, ambaye ni mbobezi wa sheria, akijibu swali hilo katika mkutano huo uliofanyika jijini Seattle- Marekani, alisema bado vyombo husika vinaendelea kutekeleza majukumu ya kuwasaka wahalifu hao.
Alisema uchunguzi wa baadhi ya matukio ni mgumu hivyo huhitaji muda mrefu zaidi kuukamilisha na hali hiyo si kwa Tanzania pekee.
“Hapa Marekani mlipo, Rais John F Kennedy na ndugu yake walipigwa risasi, lakini pamoja na teknolojia waliyonayo hadi leo waliofanya uhalifu huo hawajakamatwa,” alisema Profesa Kabudi.
Alisema Lissu ni ndugu yake na alisoma darasa moja na kaka yake ambaye ni wakili maarufu jijini Arusha, Alute Mughway na watoto wake wanamwita Alute baba mkubwa.
“Katika mapambano ya kiuchumi siyo kila jambo la kulitafutia majibu haraka.”
Baada ya majibu hayo ya Profesa Kabudi, Lissu naye aliibuka na kumjibu kupitia ujumbe uliosambazwa katika mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia jana akisema, “nimesikia alichokisema kaka yangu Profesa Palamagamba Kabudi juu ya jaribio la mauaji dhidi yangu la Septemba 7.”
“Sijashangazwa na alichokisema Profesa Kabudi. Ninamfahamu vyema baada ya kumtazama kwa karibu miongo mitatu. Kabudi ni profesa wa sheria (bahati mbaya yangu sikuwahi kuwa mwanafunzi wake) na msomi na mwerevu sana.” Alisema mtu asipomfahamu vyema, “anaweza kukulisha ‘matango pori’ kwa usomi wake, huku ukidhani amesema ukweli mtupu.”
Lissu alisema Profesa Kabudi anathibitisha ‘matango pori’ aliyowalisha wasikilizaji katika mkutano wake nchini Marekani kuhusu marais wa Marekani waliouawa na wauaji wao kutojulikana mpaka leo.
“Rais John Fitzgerald Kennedy, Rais wa 35 wa Marekani aliuawa na Lee Harvey Oswald Novemba 23, 1963. Alikuwa Rais wa nne wa Marekani kuuawa akiwa ofisini. Oswald alikamatwa na kuuawa na Jack Ruby, askari wa FBI siku hiyo hiyo,” alidai Lissu.
Alisema Rais wa kwanza kuuawa nchini humo alikuwa Abraham Lincoln, Aprili 14, 1865.
“Muuaji wake John Wilkes Booth alitoroka, lakini aliuawa baada ya kutafutwa kwa siku 12.”
Baada ya kutoa orodha ya marais wa Marekani waliouawa na waliotekeleza mashumbulizi hayo kutiwa nguvuni, Lissu alisema, “taarifa zote hizi ziko mitandaoni na Profesa Kabudi angeweza ku-google (kuzitafuta) na kupata cha kusema ukweli.”
Hata hivyo mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Sweden, Olof Palme pia yamebaki gizani, licha ya kuuawa zaidi ya miaka 30 iliyopita. Olof aliuawa Februari 28, 1986 baada ya kushambuliwa kwa risasi akitoka sinema na mkewe Lisbet Palme katikati mwa Jiji la Stockholm. Licha ya mtuhumiwa Christer Pettersson kukamatwa, lakini alisafishwa na mahakama kutohusika na mauaji hayo mwaka 1988. Kifo cha waziri huyo kimeacha maswali mengi bila majibu kutokana na uchunguzi kutofanikiwa kupata taarifa za muuaji wala sababu za kuuawa kwake.
Maoni ya wachambuzi
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema: “Nadhani katika nchi yetu watu hawako tayari kufuatilia matukio yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu.
Alisema, matukio ni mengi likiwamo la Lissu kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.
“Kama hilo la Lissu na lile la Azory (Gwanda-mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi aliyetoweka tangu Novemba mwaka jana) ambayo yanatokea na hatujui hatima yao, (huo) ni ukiukiwaji wa haki za binadamu unaopaswa kuchukuliwa hatua.”
Ole Ngurumwa alisema, “huwezi kufananisha mabaya ya nchi zingine, (Profesa Kabudi) angeweza kutoa sababu za watu kupotea kama Azory na wengine, na si kusema mbona nchi fulani haijafanya, mimi naona waziri alikosea kwani huwezi kurithi makosa ya nchi nyingine.”
Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema: “Matukio ya Marekani ni tofauti na lile la Lissu lililotokea mchana kweupe eneo lenye ulinzi. Mbona kunatokea matukio ya ajabuajabu na wahusika wanakamatwa kwa nini hili limewashinda.”

Comments