Jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiliitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea kusudi lake la kuwahamisisha wananchi kufuata uzazi wa mpango kwa sababu ndiyo sera ya Taifa.
Akizungumza katika mkutano huo, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji alisema, “Hakuna nchi yenye maendeleo ambayo haifuati uzazi wa mpango, Tanzania inakuwaje ikatae suala hili? Tutaonekana watu wa ajabu kwa mataifa yaliyoendelea,” alisema Dk Mashinji.
Juzi na jana, vyombo mbalimbali vya habari vya nje navyo viliripoti juu ya kauli hiyo ya Rais Magufuli aliyoitoa Septemba 9 akiwa wilayani Meatu, mkoani Simiyu.
Hata hivyo, baadhi ya vyombo hivyo vimeonekana kuripoti tofauti na alichokisema kwani baadhi vimedai kwamba amewataka wanawake kutotumia vidonge vya uzazi wa mpango, vingine vikiripoti kwamba, amepiga marufuku matumizi ya vidonge hivyo.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), liliripoti taarifa hiyo kwenye jarida lake la mtandaoni kwamba, Rais Magufuli amewataka wanawake kuacha kutumia dawa za uzazi wa mpango kwa sababu nchi inahitaji watu wengi.
Habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho, “Rais wa Tanzania, Magufuli apiga marufuku uzazi wa mpango,” inaonyesha kwamba Rais Magufuli alikuwa akizungumza na wanawake pekee, jambo ambalo si kweli.
Mtandao wa CNN kwa upande wake, umeripoti habari hiyo iliyokuwa na kichwa kisemacho, “Msitumie vidonge vya uzazi wa mpango; Rais wa Tanzania awaambia wanawake nchini humo.”
Akitoa ufafanuzi kuhusu kauli hiyo, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alisema alichokisema Rais kiko wazi kwamba, haoni haja kwa Watanzania kutumia uzazi wa mpango.
“Hao watu wa nje achana nao kwa sababu alichokisema kiko wazi na alielezea mtazamo wake,” alisema Dk Abbasi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo).
Akizungumza na wananchi huko Meatu, Rais Magufuli alisema yeye siyo muumini wa uzazi wa mpango na kama mwananchi anao uwezo wa kuzalisha mali, haoni sababu ya kuambiwa asizae.
Aliwataka wananchi wafanye kazi kwa bidii ili waweze kuzaa na kulisha watoto wao. “Kinachotakiwa Watanzania ni kuchapa kazi ili watoto utakaowazaa uwalishe. Wale ambao hawafanyi kazi, wavivuwavivu, ndiyo watakaojipangia watoto. Analima mwaka mzima anategemea kamnazi kamoja.
“Limeni, fanyeni kazi. Ukiwa na chakula cha kutosha, zaa. Taifa lisipokuwa na watu wa kufanya kazi, Taifa hilo halipo. Tunahitaji nguvu kazi ya Taifa letu,” alisema Rais Magufuli.
Alitoa mfano wa nchi moja ambayo asilimia 60 ya watu wake ni wazee wa kuanzia miaka 60 hadi 100 kwamba ilikuwa na sera ya kuzaa mtoto mmoja lakini sasa inapata shida ya nguvu kazi na vijana hawataki kuzaa. Alisisitiza kwamba mwenye uhakika wa chakula asipangiwe uzazi na watu wengine.
Comments