
Akizungumzia kwa ufupi juu ya hotuba hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq alisema Guterres pia
atazungumzia kuhusu masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi
na kusisitiza kuwa watu wote lazima wanufaike na tekinolojia mpya.
Aidha
atatoa mwito kwa viongozi wa kidunia juu ya haja ya kushikamana kwa
ajili ya kudumisha amani pamoja na kuheshimu haki za binadamu.
Jumla
ya viongozi 133 wa dunia wanatarajia kuhudhuria mkutano wa mwaka huu
wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa utakaomalizika Oktoba 1, likiwa ni
ongezeko kulinganisha na viongozi 114 waliohudhuria mkutano wa mwaka
jana. Hata hivyo nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zitawakilishwa
katika mkutano huo na baadhi yake zikiwakilishwa na mawaziri.
Katika
kuelekea mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa
akizungumzia dhidi ya kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo, na haja ya
kufanyika mageuzi katika siasa za kimataifa hususan katika kipindi hiki
ambacho hayajawahi kuhitajika kama yanavyohitajika sasa.
Viongozi
wanaofuta siasa kali za kizalendo wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo
ni pamoja na rais Donald Trump wa Marekani, rais wa Poland Andrzej Duda,
waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte pamoja na mawaziri wa mambo ya nje
wa Hungary na Austria.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa
Mataifa Nikki Haley aliwaeleza waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa
rais Donald Trump anayepigia upatu sera ya " Marekani Kwanza"
atazungumzia juu ya kulinda utaifa wa Marekani wakati atakapohutubia
mkutano huo muda mfupi mara baada ya Guterres kutoa hotuba yake.
Wakati
wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kujadili amani sambamba na
kuadhimisha miaka 100 ya kiongozi aliyeoongoza harakati za kupinga
ubaguzi nchini Afrika Kusini hayati Nelson Mandela waziri wa mambo ya
nje wa China Wang Yi alionya kuwa siasa kali za kizalendo na sera za
kuyahami masoko zinazidi kuongezeka.
China na Marekani katika
miezi ya hivi karibuni zimekuwa katika hali ya vita ya kibiashara huku
nchi zote mbili zikitoza viwango vikubwa vya kodi kwa bidhaa kutoka
pande zote mbili.
Masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na yale
yanayohusiana na migogoro, maeneo yanayokabiliwa na wasiwasi wa
kiusalama yanatarajiwa kujadiliwa pembezoni mwa mkutano huo wa baraza
kuu la Umoja wa Mataifa.
Mgogoro wa Syria uliodumu miaka saba
sasa, mgogoro wa Yemen uliosababisha janga la kibinadamu pamoja na
maeneo mengine barani Afrika yaliyo katika wasiwasi wa kiusalama ikiwa
ni pamoja na Libya, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati , Mali na
Congo huenda pia yakachukua nafasi katika mkutano huo.
Comments