Dkt. Shein atuma salamu za pongezi kwa Rais wa China Xi Jinping.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya Watu wa China  Xi Jinping kwa  kutimiza miaka 69 tokea kuundwa kwa Taifa hilo.
Dk. Shein, alieleza kuwa  kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar wanatoa pongezi kwa Rais Xi, wananchi wa China pamoja na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kutimiza umri huo wa Taifa hilo tokea kuasisiwa kwake.
Salamu hizo zilieleza kuwa Watu wa Zanzibar wanapata faraja na matumaini kutokana na maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana katika Taifa hilo la  China kwenye sekta mbalimbali za maendeleo na uchumi.
Aidha, salamu hizo zilieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wataendelea kutoa ushirikiano sambamba na kuimarisha uhusiano mkubwa uliopo kati yao na ndugu zao wa China.
Pamoja na hayo, salamu hizo za pongezi zilimtakia afya njema na mafanikio ya muda mrefu Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jimping katika kuliongoza Taifa hilo.
Uhuru wa Taifa hilo ulitangazwa mnamo Oktoba 1, 1949.
Zanzibar24.

Comments