WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amezindua uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu
unaojengwa na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na amezitaka wilaya
nyingine kuiga mfano huo.
Uwanja
huo unaoitwa Majaliwa umezinduliwa kwa mechi kati ya timu ya wilaya ya
Ruangwa ya Namungo FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza na timu ya
Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo ndio mabingwa wa ligi kuu Tanzania
Bara, 2018/2019.
Waziri
Mkuu amezindua uwanja huo jana (Jumamosi, Agosti 11, 2018), ambapo
ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na wananchi kwa kushiriki
kikamilifu katika ujenzi huo.
Uwanja
huo unajengwa katika kitongoji cha Mtichi kata ya Nachingwea na ndio
utakaokuwa unatumiwa na timu ya Namungo FC kuchezea mechi za nyumbani.
Amesema
suala la ujenzi wa uwanja ni jambo muhimu na hata Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) linahamasisha ujenzi wa uviwanja katika ngazi za mikoa na
wilaya ili kutoa fursa kwa wananchi hususani vijana kushiriki katika
michezo, hivyo amezitaka halmashauri nyingine ziige mfano wa wilaya ya
Ruangwa.
Akizungumzia
kuhusu mechi ya kirafiki kati ya timu za Simba na Namungo, Waziri Mkuu
amesema “Michezo ni burudani na wananchi wanataka kuburudika, Simba
chapeni kazi onesheni uwezo wenu wa mwisho ili Namungo nao waweze kupata
ufundi,”.
Pia
amesema mbali na kucheza na Simba, timu hiyo ya Namungo inatarajiwa
kucheza na timu ya Dodoma FC ya jijini Dodoma keshokutwa (Jumatatu,
Agosti 13, 2018). Pia timu hiyo itacheza na timu za Yanga na Azam za
jijini Dar es Salaa hivi karibuni.
Waziri
Mkuu ametaja faida ya timu kama za Simba, Yanga, Azam na Dodoma FC
kucheza na timu ya Namungo FC kuwa ni pamoja na kuwaimarisha wachezaji
kwa kuwafanya wajiamini na kuondoa uoga wa kupambana na timu nyingine.
Aidha,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza timu ya Namungo FC kwa hatua
waliyofikia, kwani ilianza kwa kushiriki mashindano ya kugombea kuku,
mbuzi na ng’ombe na sasa inashiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara.
“Hakikisheni mnafikia lengo letu la kucheza ligi kuu,”.
Naye,
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi amesema kutokana na jitihahada
za kuboresha maendeleo zinazofanywa na Mbunge wa jimbo la Ruangwa
ambaye ndiye Waziri Mkuu, uongozi wa mkoa umeamua kuupa uwanja huo jina
la Majaliwa ili kumuenzi.
Kwa
upande wake, Msemaji wa Timu ya Simba, Bw. Haji Manara amesema timu
hiyo ipo Ruangwa na benchi lake lote la ufundi wakiwemo wachezaji 27 na
kwamba ameshangazwa na wingi wa watu waliojaa uwanjani hapo.
“Hakuna
uwanja Tanzania unaoweza kujaza watu 20,000 kwa mechi za kawaida nje ya
Dar es Salaam na Mwanza. Nimeambiwa kulikuwa na tiketi 20,000 ambazo
zimeisha zote,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.
Mpekuzi.
Comments