WAZIRI
wa Nishati, Dk. Merdad Kalemani, amewataka wakandarasi wote nchini
wanaotekeleza mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III),
kuhakikisha wanaweka umeme katika nyumba zote zikiwamo za tembe huku
akipiga marufuku kurukwa.
Akizungumza
wakati akiwasha umeme katika vijiji vya Lukungu, Nyakaboja na Bukabile
vilivyoko Wilaya ya Busega, Simiyu, alisema wamekuwa wakipata taarifa za
wakandarasi waliopewa kazi ya kutekeleza mradi huo kuwa wamekuwa
wakiziruka nyumba hizo kwa madai hazifai kupata huduma hiyo.
Aliwataka
wakandarasi hao kuhakikisha wanapeleka umeme katika kila kijiji na kila
kitongoji ili wananchi waweze kuondokana na adha kubwa wanayokumbana
nayo ya kukosa nishati ya umeme.
“Nimepata
taarifa kuwa wananchi wenye nyumba za tembe wanarukwa, maagizo yangu ni
marufuku kuruka nyumba ya tembe, tena nyumba hizo zipewe kipaumbele cha
kwanza kupata umeme na hakuna kuruka kijiji, kitongoji au nyumba
yoyote,” alisema Kalemani.
Alisema
Serikali haitaongeza muda, siku wala saa kwa mkandarasi yeyote
atakayeshindwa kutekeleza mradi huo kwa muda mwafaka waliopewa na
Tanesco na aliwataka kutekeleza mradi huo hadi kukamilika kwake kwa muda
mwafaka.
Alisema
mkandarasi White City anayetekeleza mradi huo Simiyu kasi yake ni ndogo
na alimtaka kuongeza kasi zaidi ili kuhakikisha vijiji 152 mkoani humo
vinapata umeme.
Alisema
katika Wilaya ya Busega kupitia mradi huo vijiji vyote 54 vilivyoko
wilayani humo vitapata umeme na aliwataka wananchi kuhakikisha wanalipia
gharama ya Sh 27,000 ili kupatiwa huduma hiyo.
Pia
alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunga mfumo wa umeme
katika taasisi za umma zikiwemo shule na vituo vya kutolea huduma za
afya.
“Wakati
sisi tukihangaika kuleta umeme kwa kila mwananchi, niwatake wakurugenzi
wa halmashauri pamoja na madiwani kupitia vikao vyao, watenge bajeti
kuhakikisha taasisi zote za umma zinafungiwa mfumo mzima wa umeme kwa
ndani,” alisema Kalemani.
Awali,
Mbunge wa Busega, Dk. Rafel Chegeni, alisema bado kuna baadhi ya
vitongoji na vijiji vimerukwa na mkandarasi anayetekeleza mradi huo.
Dk.
Chegeni alisema kilio kikubwa cha wananchi wa jimbo hilo ni ukosefu wa
umeme na alimwomba Kalemani kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda
mrefu.
Mpekuzi.
Comments