MKURUGENZI
wa Benki ya Rasilimali(TIB) Bw. Charles Singili amesema kuwa
watashirikiana na taasisi nyingine za fedha ili kuhakikisha wanaunga
mkono juhudi za Rais Dk.John Magufuli katika kuinua sekta ya kilimo
nchini.
Ametoa
kauli hiyo jana wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati wa tukio la
kukabidhiwa kwa matrekta 10 yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango
kwa Chuo cha Kilimo(SUA) cha mkoani Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa
ahadi ya Rais kwa chuo hicho.
Alisema
TIB inatambua na kuthamini jitihada za Rais kwenye kuinua kilimo nchini
na wao wanalo jukumu la kuhakikisha malengo na mikakati ya Serikali
inafanikiwa.
Alifafanua
kwamba TIB wanashukuru kwa kujumuishwa kwenye tukio hilo la kukabidhiwa
matrekta hayo kwa SUA hasa kwa kuzingatia nao ni wadau muhimu katika
eneo la kilimo.
Aliongeza
kuwa Serikali ilifanya uamuzi wa kuanzisha dirisha la kilimo mwaka 2009
ikiwa ni maandalizi ya kuanzisha benki ya kilimo na ilitenga Sh.bilioni
42 ambayo nia yake ilikuwa kuanza kuchochea ukuzaji wa kilimo.
Alifafanua
baada ya kuanzishwa benki hiyo moja ya eneo ambalo walijikita ni kwenye
zao la pamba na kwamba wanao ujuzi wa kutosha kwenye eneo la
ukopeshaji hasa katika zana za kilimo.
“Kutokana na uwezo huo tulifanikiwa kutoa mkopo katika eneo hilo na zana za kilimo ambapo tumekopesha matrekta 249.
“Na
bahati nzuri chini ya Wizara yako (Wizara wa Fedha) ipo na Benki
Kuu(BoT) na kuna sheria inayotuongoza katika kutekeleza vema majukumu
yetu,”alisema Singili.
Alisema
kutokana na uwepo wa sheria hiyo wamekuwa na utaratibu mzuri wa utoaji
mkopo wa zana za kilimo ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea baadhi ya
changamoto.
Singili
alisema changamoto ya kwanza ni ile ambayo ilikuwa inatokana na
kukosekana kwa mzunguko unaohitajika ambao ni uwepo wa kiwanda cha
matrekta na hivyo kubaki na mzunguko benki ambayo ni mkopeshaji pamoja
na mkopaji.
Alisema
juhudi za Serikali za kuhakikisha kuna kuwa na kiwanda hicho
kumekamilisha mzunguko unaotakiwa kwani sasa kutakuwa na mwenye kiwanda,
benki na mkopeshwaji.
“Unapokuwa
huna mwenye kiwanda ambaye ndiye mtengenezaji wa zana za kilimo maana
yake inapoharibika hasara inabaki kwa anayetoa mkopo na aliyekopeshwa.
“Kwa
sasa hata trekta linapoharibika inakuwa rahisi kwani aliyetengeneza
yupo hivyo hakutakuwa na changamoto ambayo ilikuwa awali,”alisema
Singili.
Alitaja
changamoto nyingine iliyokuwepo ni ubora wa zana za kilimo ambayo nayo
ilisababisha chombo kinapoharibika basi mkopaji anashindwa kulipa mkopo
na matokeo yake benki inakuwa kwenye wakati mgumu ambapo kwa sasa hilo
nalo limepata ufumbuzi wake.
Alitumia
nafasi hiyo kueleza kwamba uwepo wa matrekta hayo usiwe tu kwa ajili ya
kutumika kulima na kuvuta bali sasa yatumike katika kuongeza thamani
ya mazao ya mkulima ili naye anufaike.
Alifafanua
kwamba injini ya trekta inapozunguka inaweza kufanya kazi za zaidi ya
moja kwani mashine hizo zikiungwanishwa na mashine nyingine inaweza
kutumika kwa kufanya kazi nyingine.
“Ni
wakati sasa wa kutazama na kuhakikisha injini ya tekra inatumika kwa
kufanya mambo mengine kwa lengo la kumuwezesha mkulima kuongeza thamani
ya mazao yake,”alisema Singili.
Alisisitiza
ameona kuna trekta zenye puli zaidi ya moja na hivyo badala ya kulima
na kuvuta trekta likiwaka linaweza kutumika kwa ajili ya shughuli
nyingine.
Alitumia
nafasi hiyo kumueleza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto
James kwamba wapo tayari kushirikiana na taasisi nyingine kufanikisha
malengo hayo.
Alisema
mahitaji ya nchi ni matrekta milioni 2 na unapoangalia gharama yake ni
kubwa hivyo ili kufanikisha inahitaji nguvu ya pamoja.
Mpekuzi.
Comments